SERIKALI YAIPONGEZA KAMPUNI YA PETROBENA KWA KUSAMBAZA MBOLEA ZA TUMBAKU KWA WAKATI.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO DR MARY MWANJELWA KULIA AKIPATA MAELEZO KUHUSU MBOLEA YA TUMBAKU INAYOZALISHWA NA YARA NA KUSAMBAZWA NA KAMPUNI YA PETROBENA KATIKA GHALA LILILOPO MJINI TABORA

TABORA
SERIKALI imeipongeza kampuni  ya PETROBENA ambao ni wasambazaji wa mbolea za YARA kwa kusambaza mbolea ya tumbaku kwa wakati katika mikoa ya kitumbaku Tabora,Kahama,Kigoma na Mbeya hali itakayowawezesha wakulima kuandaa kilimo chao kwa kufuata kalenda sahihi ya zao hilo.

Wito huo umetolewa jana mjini Tabora na Naibu waziri wa Kilimo Dr Mary Mwanjelwa katika uzinduzi wa Ghala la kuhifadhia mbolea za YARA uliofanyika katika viwanjwa vya Reli mjini Tabora (TRC).

Dr Mwanjelwa amesema kuwa Kampuni ya usambazaji  wa Pembejeo ya PETROBENA imefanya jambo jema na la kizalendo kwa kuwafikishia wakulima mbolea kwa wakati na kwamba walichokifanya ndicho ambacho serikali inakitaka kifanyike na kuigwa na wauzaji wengine wa  pembejeo nchini.

Ameongeza kuwa Serikali inataka wakulima wanufaike na kilimo chao na ili wafanikiwe ni lazima mbolea ifike kwa wakati,iwe yenye ubora  na pia iuzwe kwa bei elekezi isiyomuumiza mkulima.

Akitoa bei elekezi ya mbolea aina ya NPK 10:18:24, Dr Mwanjelwa amesema kuwa mfuko wa kilo 50 uuzwe kwa Shilingi 82,000 na kwamba kila mkulima azingatie upandaji wa miti na kutumia mabani ya kisasa ili kuendelea kuhifadhi mazingira.

Naye Mkuu wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri baada ya kuwapongeza YARA na wasambazaji wao PETROBENA amewataka pia wauzaji wa pembejeo wengine mkoani Tabora kuzingatia bei elekezi na kusema kuwa kwa yeyote atakayepandisha bei serikali hatosita kumchukulia hatua kali za kisheria kwa kukiuka maagizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya PETROBENA Peter Kumalilwa amesema kuwa kampuni yao itaendelea kuunga mkono juhudi za kumkomboa Mkulima zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Raisi Dr John Pombe Magufuli kwa kusambaza mbolea kwa wakati katika maeneo yote nchini,Ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi bora na sahihi ya mbolea kulingana na mazao husika.

Awali akitoa salamu za kampuni ya YARA,Meneja mkuu wa kampuni hiyo nchini William Ngeno amesema kuwa kwa sasa wana mawakala wadogowadogo wapatao 44 katika wilaya zote za mkoa wa Tabora,na kusisitiza kuwa mbolea zote za  YARA zitamfikia mkulima kwa ubora ule ule uliotoka nao kiwandani.

Nao wakulima wa tumbaku na mahindi katika mkoa wa Tabora,Wameishukuru kampuni ya Petrobena kwa kusambaza mbolea za Yara kwa wakati na kwamba hali hiyo imewasaidia kulima na kupanda kwa wakati na kuongeza mapato ya mazao tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

MATUKIO KATIKA PICHA:
 MENEJA MKUU WA YARA TANZANIA WILLIAM NGENO AKITOA SALAMU ZA KAMPUNI KWA NAIBU WAZIRI WA KILIMO DR MARY MWANJELWA.

 MBOLEA ZA KAMPUNI YA YARA AMBAZO ZINASAMBAZWA NA KAMPUNI YA PETROBENA ZIKIWA KATIKA GHALA LA PEMBEJEO MKOANI TABORA.

 MENEJA USAFIRISHAJI WA KANDA YA TABORA (TRC) JONAS AKUMWISE AKIONGEA MBELE YA NAIBU WAZIRI WA KILIMO DR MARY MWANJELWA NA KUWASHUKURU KAMPUNI YA YARA NA PETROBENA KWA KUWA WATEJA WAO WAKUBWA NA KULIONGEZEA MAPATO SHIRIKA HILO.


 MMOJA WA WAKULIMA WA TUMBAKU KUTOKA WILAYA YA URAMBO AKITOA USHUHUDA KUHUSU NAMNA MBOLEA ZA YARA ZILIVYOMSAIDIA KUPATA MAZAO MENGI KATIKA MSIMU ILIOPITA.

 NAIBU WAZIRI WA KILIMO DR MARY MWANJELWA KUSHOTO AKIFUNGUA RASMI GHALA LA KUHIFADHIA MBOLEA ZA YARA LILILOPO MJINI TABORA,KULIA NI MKUU WA MKOA WA TABORA AGGREY MWANRI.


 NAIBU WAZIRI WA KILIMO DR MARY MWANJELWA AKIKAGUA BANDA LA WAKULIMA NA KUJIONEA MAZAO YALIYOSTAWISHA NA MBOLEA ZA YARA ZINAZOSAMBAZWA NA KAMPUNI YA PETROBENA.

 NAIBU WAZIRI WA KILIMO DR MARY MWANJELWA KUSHOTO AKIPATA MAELEZO YA SHUGHULI ZINAZOFANYWA NA KAMPUNI YA YARA KUTOKA KWA BWANA SHAMBA NA AFISA MASOKO WA KAMPUNI YA YARA KWA MIKOA YA MWANZA,TABORA NA KIGOMA BWANA FOCUS LAURENT.


BAADHIYA WAKULIMA WA MKOA WA TABORA WAKIMSIKILIZA KWA MAKINI NAIBU WAZIRI WA KILIMO DR MARY MWANJELWA (HAYUPO PICHANI)
SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata