YAJUE USIYO YAJUA KUHUSU MJI WA SUMBAWANGA NA HISTORIA KUHUSU UCHAWI

NI majira ya saa 10:30 alasiri hali ya hewa ikiashiria mawingu ikiwa ni dalili za kunyesha mvua,angani upande wa mashariki kulikuwa na alama ya upinde wa mvua uliopambwa kwa rangi anuai katika anga hilo sanjari na jua jepesi lililokuwa likishindana na mvua iliyokuwa ikitaka kunyesha wakati huo.
Bodaboda,  usafiri niliotumia kufika hapo, dereva wa boda boda aliniondoa hofu kutokana na wingu lililotanda angani huenda lingeweza kunitotesha mwili wangu na kunieleza uzoefu wake kuwa kutokana na dalili hizo angani mvua haiwezi kunyesha.
Nilishuka na kumlipa dereva wa  bodaboda na kukatisha katika mitaa ya mji wa Sumbawanga ambao wenyeji waliniambia kuwa hapo ndipo lilipo jina halisi la Sumbawanga. 

 'Sumbawanga Wenyeji' ndilo jina halisi la eneo hilo, mji wake ulipangwa vyema na mitaa yake ilionesha kuzingatia ramani za mipango miji tofauti na ilivyo baadhi ya miji mingi mikubwa ambayo nyumba zake zimejengwa holela holela bila kuzingatia ramani za mipango miji.
Ukale wa nyumba hizo unaonekana dhahiri katika paa la nyumba hizo ambazo asilimia kubwa bati zake zinaonekana zikiwa zimefifia na kutengeneza kutu na rangi nyeusi ilhali kuta za nyumba za mitaa hiyo zikionekana kuchakaa,dalili pekee ya kuwa nyumba hizo zimejengwa miaka mingi iliyopita.

Kwenye baadhi ya nyumba mbele ya vibaraza vya nyumba hizo kulikua na akina mama walioketi baadhi yao wakisukana nywele,wengine wakichambua mboga huku baadhi yao wakipiga soga kama ilivyo desturi ya mitaa mingi ya maeneo ya mijini.

Mbele yangu navutiwa na jumba kubwa imara na chakavu lililotelekezwa ambalo linaonekana ni jumba la kale kuliko nyumba nyingi zinazozunguka maeneo hayo, baadhi ya nyumba zilizopo jirani ya jumba  hilo zikiwa ndogo ndogo tofauti na jumba hilo kuu na kuu kuu.

Jengo hilo limejengwa kwa ustadi mkubwa na matofati madogo madogo ya kuchoma likiwa na nguzo kubwa na imara eneo la juu karibu na paa likiwa mithili ya nyumba ya kifalme sawa na nyumba za kale zilizopo maeneo ya Bagamoyo, Kilwa na Zanzibar.

Natupia macho mbele yangu nakutana uso kwa uso na mwanamama aliyekuwa akistaajabu mshangao wangu, nikasogea karibu yake na kumuamkia kwa heshima kulingana na umri wake. 

Nilimkadiria mama yule umri wake ni kati ya miaka 75 na 80 lakini akionekana bado mwenye nguvu za kutosha 

Georgina Noel Kamzee(71)ndilo jina la Bibi huyu nilikosea kidogo kumkadiria umri wake lakini kulingana na maelezo ya mwanaye wa kike aliyeambatana naye akijitambulisha kama mtoto wa mama huyo anasema kuwa mama yake amezaliwa miaka 71 iliyopita kulingana na takwimu alizonazo katika vyeti vya kuzaliwa.
Nilishawishika kumuuliza nilichokuwa nakishangaa eneo lile na kumuuliza kwanini jengo lile liko pale na lipo kwa matumizi gani.

Bi. Kamzee ananisimulia machache kulingana na jinsi anavyolifahamu jumba lile kwa kusema kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliozaliwa pale na kukulia hapo na kuwa Jumba hilo ni mali ya familia ya Mamwene 'Machifu wa eneo hilo la Sumbawanga'.

Anasema kuwa wakati akiwa binti mdogo jumba hilo lilikuwa zuri lenye kuvutia ambapo kiongozi wa kabila la Wafipa alikuwa akiishi hapo pamoja na wafuasi wake.
Anasema kuwa anakumbuka kuwa mahala hapo alikuwa akiishi mwanamke ambaye ndiye alikuwa mtawala wa eneo hilo aliyefahamika kwa jina la Mwene Ngalu aliyezaliwa kutokana na Mwene Wakulosi.

Anasema kuwa wapo wanafamilia ambao ndio warithi wa utawala wa kichifu ambao hadi sasa wangalipo na kuwa utawala wao ulikuwa ni wa kurithishana kulingana na wakati na enzi lakini baada ya wakoloni kuondoka na kupatikana Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 zama za utawala wa kichifu ulimalizika.

''Hivi sasa Umwene umebaki kwa wanafamilia wenyewe utawala wao ulikoma baada ya Nyerere kuingia madarakani,''anasema Bi. Kamzee.

Anasema kuwa ndani ya jumba hilo yapo makaburi ya Mamwene wa Kabila la Wafipa ambao walizikwa humo kuanzia Mwene wa Kwanza Mwene Ngalu.

Engebert Wangao ni mjukuu wa Mwene Ngalu anasema kuwa jumba hilo limebaki kama kumbukumbu ya kifamilia na sehemu ya kuwazika viongozi wao wa kiukoo na kwamba ijapokuwa ndilo lenye historia yote ya kabila la Wafipa serikali haijaona umuhimu ya kuitunza kumbukumbu hiyo kwa historia ya vizazi vijavyo.

Anasema kuwa ndani ya jumba hilo kuna makaburi ambapo wamezikwa Mwene Ngalu ambaye alikuwa ni mwanamke aliyeolewa na Wangao Kapufi ambaye aliwazaa akina Joseph Kapufi,na Adolf Kapufi ambaye ni mzee pekee aliyebaki katika wajukuu wa Mwene Ngalu na mzee Wangao Kapufi. 

Adolf Wangao Kapufi(85) ni mtoto wa Chifu Kapufi Wangao, Wangao ni mume wa Mwene Ngalu aliyekuwa mtawala mwanamke wa Kabila la Wafipa walioishi eneo la Sumbawanga.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mzee Adolf Wangao ambaye alikuwa akizungumza kwa msaada wa mwanaye Saimon Wangao Kapufi,kutokana na hali yake ya afya kuzorota kwa ajili ya uzee, anasema kuwa baba yake ndiye Kiongozi wa Kimila aliyebaki na ndiye aliyeshikilia mikoba ya kabila la wafipa kwa sasa.

Anasema kuwa historia ya Mwene Ngalu inatokana na familia mbili za babu zao. ambapo baba yao Mwene Ngalu na mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Mwene Wakuling'anga walizaliwa nchini Ruanda baada ya baba yao kuhamia huko na kuoa mwanamke wa kabila la kitutsi na kuzaa watoto watatu wa kike.

Anasema kuwa baada ya kuishi huko kwa miaka mingi waliamua kurejea kwenye makazi yao ambapo wakiwa njiani kupitia nchini Zambia mmoja wao alibaki nchini Zambia na wao wakaamua kurejea hadi katika makazi yao na himaya ya baba yao.

Kulingana na maelekezo ya baba yao ambapo walipofika walimkuta baba yao mdogo aliyetambulika kwa jina la Chatapwa aliyemiliki eneo lote lililokuwa mji wa baba yao.
Kulingana na maelezo kwa mujibu wa historia ya milki ya kabila la wafipa.
 Inasemekana kuwa  baba yao mdogo aliyefahamika kwa jina la Chatapwa alikuwa na nia ya kuwadhulumu mabinti wale eneo waliloachiwa na baba yao ndipo walipoamua kufika eneo la mlimani ili kuona mipaka ya ardhi yao waliyoachiwa na baba yao.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyokutwa na vizazi hivyo ni kwamba, Chatapwa ambaye ni baba mdogo wa mabinti hao alikuwa ana nywele nyingi za kwapani hivyo alipotakiwa kuonesha mipaka ya ardhi yake alishindwa kuinua mikono yake kwa kuhofia kuonekana kwa nywele zake za kwapani hivyo akainua mikono yake na kuonesha eneo la mipaka ya ardhi yake kwa karibu.

Wale Mabinti walipoona baba yao mdogo kaonesha ukubwa wa ardhi kulingana na eneo hilo wao walinyanyua mikono yao na kuonesha umbali mkubwa na hivyo kupata fursa ya kuchukua eneo kubwa la ardhi na wao kutawazwa kuwa ndio wamiliki wa eneo lote la milima ya Ufipa kwenye mji wa Milanzi.

Baada ya kutawazwa kuwa na miliki hiyo dada mkubwa Mwene Ngalu alihamia eneo hilo lenye jumba la zamani la makumbusho na kuwa katika maisha yake ya kawaida walikuwa wakija wachuuzi wa biashara waliokuwa wakileta zawadi mbalimbali kwa Mwene Ngalu miongoni mwa wachuuzi hao alikuwepo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Wangao.

Wangao kama walivyo wachuuzi wengine baada ya kumaliza biashara zake na kutaka kurejea nyumbani kwake alizuiwa na Mwene Ngalu na ndipo ilipokuwa mwanzo wa yeye kuishi na Mwene Ngalu kama mtu na mkewe.(rejea kitabu A State In The Making Myth History and Social Transformation In Pre-Colonia Ufipa. 
kilichoandikwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa wilaya wakati wa Utawala wa kikoloni aliyefahamika kwa jina la Roy Willis).

Kwa mujibu wa Adolf Wangao ni kwamba historia ya kabila wa Wafipa miliki ya Kabila la Ufipa ilikuwa ikilindwa na Mamwene wadogo waliokuwa wakiishi jirani na Jumba kuu la Mwene na kuwa desturi ya watu wa kabila hilo walikuwa ni waaminifu ambao hawakuwa wadokozi kwa mali za watu wengine.

Anasema kuwa watu wa makabila mengine tofauti na kabila la Wafipa walikuwa wakija kutaka kuiba mali kwa njia ya nguvu za giza hali ambayo iliwafanya waanze kujilinda kutokana na watu ambao hawakuwa na nia njema na wakazi wa maeneo hayo.

Kulingana na tabia hiyo wakazi wa eneo hilo ambalo awali lilikuwa likifahamika kwa jina la Isachi waliwataka wageni wanaoingia katika mji huo kabla ya kuvuka mto watupe Uchawi ndipo waingie katika mji huo wakiwa wasafi.

Neno hilo la TUpa Uchawi kwa kabila la Kifipa lilikuwa na maana ya 'Sumba Wanga'hivyo kila aliyeingia katika mji huo alitakiwa kuutupa uchawi wake mtoni kabla ya kuingia katika mji huo.

Inadaiwa kuwa wapo waliokiuka masharti na kukutwa na madhara makubwa na ndio sababu hasa la hekaya zinazoelezwa kuwa asili ya watu wa mji huo ni Wachawi.

Kulingana na maelezo ya Mwene Adolf Wangao ni kwamba historia na maelezo mengi yanayouelezea mji wa sumbawanga kuhusisha na imani za Uchawi hazina ukweli bali historia hiyo inarudi miaka ya nyuma kutokana na tabia za wageni waliokuwa wakitumia uchawi dhidi ya wenyeji wa kabila la Wafipa.

''Kwa umri wangu sijawahi kusikia wala kuona vituko vya uchawi, watu wanaogopa tu, hii ni historia iliyopo kulingana na matukio ya watu waovu waliokuwa wakiwafanyia hila watu wa kabila letu,''anasema Mzee Adolf Wangao ambaye ndiye mrithi wa mikoba ya wanaukoo wa kichifu wa kabila la Kifipa.

Wilaya ya Sumbawanga ambayo ndiyo makao makuu ipo mkoa wa Rukwa ambao ni moja kati ya mikoa 30 ya Tanzania, inayopakana na mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi, Upande wa Kaskazini, mkoa wa Mbeya upo upande wa Mashariki ambapo nchi ya Zambia ipo upande wa kusini na upande wa magharibi lipo Ziwa Tanganyika ambalo lipo mpakani mwa nchi ya DRC.

Kabla ya kugawanywa mwaka 2012 mkoa ulikuwa na ukubwa wa eneo kilomita za mraba 70,000 ambapo upande wa kusini mwa mkoa huo lipo Ziwa Rukwa moja ya maziwa makubwa yaliyopo Afrika Mashariki.
Kitabu kilichoandikwa na Mkuu wa wilaya wa enzi za Ukoloni wa wilaya ya Sumbawanga Mr. Roy Willis ambaye alikusanya historia ya kabila la Wafipa na mila zao kutoka kwa ndugu wa ukoo wa Ufalme wa Wafipa.
Mwene Joseph Kapufi
Mwene Antony Kapufi Wangao wa III mjukuu wa Mwene Ngalu

Mmoja kati ya wajukuu wa Mwene Ngalu akionesha makaburi ya Mamwene wa Kabila la KifipaMjukuu wa Mwene Ngalu, Engebert Wangao, akionesha eneo la majani ambalo ni moja ya kaburi la Mwene wa kabila la Wafipa

Eneo la Makaburi ya Machifu wa kabila la Wafipa yaliyopo kwenye nyumba ya kale iliyokuwa ikitumika zamani


Mwene Aldorf Kapufi Wangaa  IV akiwa na zana zake za Uchifu


Mwene Aldof Wangao Kapufi-IV Kiongozi wa Kimila wa Kabila la Wafipa

Mwene Ngalu(I) mwanamke mtawala wa Kabila la Wafipa

CREDIT: MWANA FASIHI MAHIRI BLOG

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata