ZAIDI YA WANAUME 35,000 MKOA WA SHINYANGA WAFANYIWA TOHARA


Na Sebastian Mnakaya
KAHAMA.

Zaidi ya wanaume 35,000 katika mkoa wa SHINYANGA wamefanyiwa tohara katika vituo mbalimbali mkoani humo katika kipindi cha Octoba mwaka jana hadi mwezi Machi mwaka huu, huku ikitarajiwa kuwafanyia wanaume 64,000 ifikapo Septemba mwaka huu.

Akizungumza leo na KAHAMA FM mshauri wa huduma za tohara kwa wanaume kutoka shirika la INTRAHEALTH INTERNATIONAL mkoani Shinyanga, Dkt ENNOCENT MBUGI amesema zoezi hilo linawalenga watoto kuanzia umri wa miaka 10 na watu wazima.

Naye mtoa huduma za tohara kwa wanaume katika hospitali ya Halmashauri ya mji wa Kahama, LINDA KIDOLEZI amesema kumekuwa na muitikio mdogo miongongoni mwa wanaume wenye umri kuanzia miakaa 20 na kuendelea ikilinganishwa na wale wa chini ya umri huo.

Kwa upande wao baadhi ya Wanaume waliofanyiwa tohara katika Hospitali ya mji wa Kahama wamesema wanajisikia fahari na kujiamini baada ya zoezi hilo kwani wana uhakika wa kuepuka maambukizi ya magonjwa ya ngono ukiwemo UKIMWI kwa asilimia kubwa.

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la INTRAHEALTH INTERNATIONAL mwaka 2010 ilianzisha kampeni hiyo ya tohara bure kwa wanaume kuanzia miaka kumi hadi miaka 60, lengo likiwa ni kuwaepusha na uwezekano wa kuambukizana magonjwa ya ngono, hususan UKIMWI.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata