TATIZO LA KUVIMBA MIGUU KWA WAJAWAZITO

Akina mama wengi wajawazito hupata matatizo ya kuvimba miguu wakati wa ujauzito kwa sababu mbalimbali ambapo wengine huwa ni hali ya kawaida kwa maana ya kwamba haisababishwi na ugonjwa wa aina yoyote na wengine hali hiyo husababishwa na magonjwa mbalimbali.

Wakati mimba inapokua kubwa tumbo la uzazi (Uterus) hukandamiza mishipa ya damu inayorudisha damu kwenye moyo (Veins) au ile mishipa inayobeba maji damu (lymph) kutoka kwenye miguu, hali inayofanya damu na maji kushindwa kurudi yote kwenye moyo na kujikusanya sehemu ambazo ni tegemezi hasa sehemu za miguuni na kusababisha uvimbaji wa miguu ujulikanao kitaalam kama ‘Dependent Oedema’.

Uvimbaji huu ni ule ambao hutokea kwenye sehemu ya chini ya mguu chini ya kifundo cha mguu (Ankle Oedema), kama miguu ikivimba kupanda juu hadi kwenye mapaja au juu zaidi hii huwa ni dalili ya ugonjwa.

Magonjwa ambayo yanaweza kusababisha uvimbe miguuni na sehemu nyingine za mwili wa mjamzito ni pamoja na kuwa na shinikizo la damu la ujauzito (Pre-eclampsia), magonjwa ya figo ambapo mtu huvimba miguu na uso pia na magojwa ya ini  yanayosababisha maji kujaa kwenye ukuta wa mbele wa tumbo (Ascites) ambapo mwili wote unaweza kuvimba pia.

Mjamzito anaweza kuvimba miguu kutokana na kuwa na ukosefu wa protini kwenye damu (Hypoproteinaemia) kwa sababu yoyote na ugonjwa wa moyo (Heart Failure).

Ni vizuri mjamzito anapovimba miguu aende hospitali kwa ajili ya uchunguzi ambapo ataweza kupatiwa matibabu kulingana na tatizo litakalogundulika na madaktari.

Endapo madaktari watagundua kuwa uvimbe huo hausababishwi na magonjwa  (Dependent Edema) anachotakiwa kufanya mjamzito ni kutosimama kwa muda mrefu na hata akikaa miguu asiining’inize lakini pia wakati wa kulala asipende kulalia mgongo (kulala chali) kwani hii husababisha mfuko wa uzazi (Uterus) kukandamiza hiyo mishipa ya damu na kusababisha uvimbe miguuni kama ilivyoelezwa hapo juu.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata