SERIKALI YASHAURIWA KUWEKA MTAALA WA SOMO LA WATU WENYE ULEMAVU WAKIWEMO ALBINO


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Serikali imeshauriwa kuweka mtaala wa somo la watu wenye ulemavu ukiwemo wenye Ualbino kwenye shule za msingi na sekondari ili kuwawezesha wanafunzi kuelewa haki za walemavu na kuondoa unyanyapaa dhidi yao.

Hayo yameelezwa katika Kata ya Bugarama Halmashauri ya MSALALA Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA, na baadhi ya washiriki wa semina ya kutathimini elimu ya watu wenye ualbino iliyoshirikisha washiriki kutoka kata za Bulyanhulu na Bugarama katika Halmashauri hiyo.

Wakichangia katika semina hiyo, DEVOTHA KAPESA na JOYCE LWANJI wamesema serikali ilitazame suala hilo kwani elimu hiyo ni muhimu kwa watoto waweze kuelewa kwamba ulemavu huo ni jambo la kawaida kwa binadamu.

Katibu wa Chama cha watu wenye ualbino Tanzania (TAS) wilaya ya Kahama, SITA MASENYA ameyaomba mashirika, taasisi mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya watu wenye ualbino ili kujenga uelewa wa kutosha kwa wananchi.

Kufuatana na takwimu za mwaka jana, Wilaya ya Kahama ina watu wenye Ualbino wapatao 96, ambapo imebainika kwamba kukosekana kwa elimu kunasababisha baadhi ya familia kuwaficha watoto wenye ulemavu huo na hata jamii kuwanyanyapaa.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata