MAMBO AMBAYO KILA MZAZI ANAPASWA KUMFUNDISHA MWANAE

Mzazi au mlezi ndiye mwalimu namba moja wa mtoto wake. Kwa kiasi kikubwa sana mtoto hujifunza na kuiga vitu au mambo mbalimbali kutoka kwa wazazi au walezi wake.

Hivyo ni muhimu sana mzazi kuhakikisha anamfundisha mtoto wake mambo muhimu anayopaswa kujifunza ili akue katika malezi bora na awe na baadaye (future) njema.

Kwa kutambua umuhimu wa mzazi au mlezi kumfundisha mtoto wake mambo kadhaa muhimu;

karibu ufahamu vitu au mambo ambayo kila mzazi au mlezi anatakiwa kumfundisha mtoto wake.

1. Matumizi mazuri ya muda
Matumizi ya muda ni swala muhimu kwa kila mtu, tena ni msingi wa mafanikio kwa kila mtu. Hivyo mzazi au mlezi anapaswa kumfundisha mtoto wake matumizi ya muda tangu akiwa mtoto ili akue akiwa na tabia hiyo.

Mzazi au mlezi anapaswa kumfundisha mtoto wake maswala kama vile kuamka mapema, kulala kwa wakati, kuwahi eneo husika kwa muda stahiki, kujiwekea ratiba na kuifuata.

2. Matumizi Mazuri ya pesa
Ni watu wachache sana ndiyo wenye matumizi mazuri ya pesa; hii inatokana na kutokujifunza kutumia pesa vyema tangu utoto wao.

Kila mzazi au mlezi anapaswa kumfundisha mtoto wake umuhimu na njia za kutumia pesa vyema.
Ni muhimu mtoto afundishwe kuweka akiba, afundishwe kununua vitu vya maana na si vitu kama pipi na biskuti, afundishwe kutumia pesa kulingana na jukumu la pesa hizo.

Kumfundisha mtoto tabia hii kutamfanya akue huku akiwa na tabia ya kutumia pesa vyema.

3. Elimu ya jinsia
Wazazi au walezi wengi hufikiri kuwa kuwafundisha watoto wao elimu ya jinsia ni kinyume na maadili au ni kuwafundisha tabia mbaya. Hili limetoa mwanya kwa watoto wao kupata elimu potofu kutoka kwa marafiki au watu wasio sahihi.

Ili kumwepushia mtoto mimba za utotoni, ndoa za utotoni au hata magonjwa ya zinaa ni muhimu afundishwe elimu ya jinsia na mzazi au mlezi wake.

4. Tabia ya kusoma vitabu
Vitabu ni chanzo cha maarifa ambacho hakiwezi kubadiliwa na kitu kingine chochote; hata maarifa mengi yaliyoko kwenye mtandao wa intaneti kwa kiasi kikubwa yamechukuliwa kwenye vitabu.

Kila mzazi au mlezi anapaswa kusoma vitabu na kumfundisha mtoto wake tabia ya kusoma vitabu ili ajipatie maarifa mbalimbali yatakayoboresha maisha yake.

5. Kumwamini Mungu
Kila binadamu ameumbwa awe na imani fulani. Imani humsaidia binadamu kwa njia mbalimbali kamavile kutawala mwenendo au tabia yake pamoja na kumpa tumaini maishani hasa wakati wa uhitaji.

Mtoto aliyefundishwa kumwamini Mungu, na akaliweka swala hilo kwenye matendo ni lazima atakuwa ni mtoto mwenye maadili mema na mafanikio lukuki.

Hivyo kila mzazi au mlezi anapaswa kuwa mfano mwema wa kumwamini Mungu, kumfundisha na kumhimiza mtoto kumwamini Mungu.

6. Kujali afya yake
Afya ni swala muhimu kwa kila binadamu, hivyo mzazi au mlezi anatakiwa kumfundisha mtoto wake kujali afya yake.

Mzazi anapaswa amfundishe mtoto kuoga, kufua nguo zake, kunywa maji safi na salama, au hata kuchukua tahadhari nyingine ili kulinda afya yake.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata