DENI LA TAIFA KUFANYIWA UHAKIKI MWAKANI

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji amesema mwaka ujao wa fedha, Tanzania itafanyiwa tathimini kuhusu deni la taifa.

Dk. Kijaji ametoa kauli hiyo bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdalah Salim (CUF) ambaye alihoji ni lini deni la taifa litafanyiwa uhakiki ili kuwe na hali nzuri ya uchumi.

“Mnaendelea kukopa na deni halifanyiwi uhakiki ni lini sasa mtafanya mkakati huu wa uhakiki kwa haraka,”amehoji.

Akijibu swali hilo, Dk. Kijaji amesema Serikali haijawahi kuacha kulipa deni hata mwezi mmoja ndiyo maana Tanzania bado inaaminiwa.

“Mikopo yote tunayokopa tunapeleka kwenye maendeleo ya kiuchumi na bado tunasisitiza kuwa deni letu ni himilivu.

“Kuhusu uhakiki wa deni letu katika mwaka ujao wa fedha itafanyiwa tathimini,”amesema.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amehoji ni lini Serikali italeta sheria bungeni ya mikopo ili inapokopa wabunge wafahamu.

Akijibu hilo, Dk. Kijaji amesema: ” Serikali tunapokopa tunafuata sheria na katiba na imeendelea kusimamia deni la taifa kwa kuzingatia sheria ya mikopo,”.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata