MBOGO AJERUHI WATU WATANO ROMBO

Watu watano, wakazi wa Kata ya Kirongo, wilayani Rombo, Kilimanjaro wamelazwa hospitali baada ya kujeruhiwa na mbogo anayesadikiwa kutoka nchi jirani ya Kenya.

Majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Karume iliyopo tarafa ya Usseri wilayani humo.

Akizungumza na Mcl Digital, leo Mei 14, Diwani wa kata ya Kirongo, Samanga Kimario amesema kuwa watu hao walikumbwa na mkasa huo wakati wakitoka kanisani jana Jumapili.

“Inasemekana walikuwa wanatoka kanisani na wakavamiwa na mnyama huyo na akawajeruhi sehemu mbalimbali za miili yao,” amesema.

Kimario amesema kuwa mnyama huyo amezua taharuki kubwa na ya kihistoria kwani haijawahi kutokea mbogo akaingia eneo hilo.

Pia amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi aliwasiliana na maofisa wanyamapori ili kupata msaada zaidi wa kunusuru maisha ya wananchi.

"Baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi kuhusiana na mnyama huyo niliwasiliana na maofisa wanyamapori ili watusaidie na baadaye walifanikiwa kumuua mnyama huyo, " amesema Diwani Kimario.
Na Janeth Joseph,Mwananchi

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata