KITWANGA AMTAKA WAZIRI WA FEDHA PHILIP MPANGO AJIUZULU

Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amesema kama Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango anadai hana fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ni vyema akajiondoa katika wadhifa huo.
Kitwanga ambaye ni mbunge wa Misungwi (CCM) ametoa kauli hiyo jana jioni Alhamisi Mei 24, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2018/19.
Mbunge huyo ameishauri Serikali kuangalia mipango ya kuanzisha miradi mikubwa ya kuzalisha umeme, kuachana na miradi midogo.
“Hivi kwanini unakosa fedha? Kama ni waziri wa fedha halafu unasema hakuna fedha ondoka hapo,” amesema.


Amesema miradi midogo ina gharama kubwa za uendeshaji ikiwemo kuwalipa mishahara watumishi wanaohudumia katika vituo hivyo na kumshauri Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani kuja na mpango wa kuzalisha umeme wa Megawati 5,000 kwa kutumia makaa ya mawe.
“Wazungu wanasema uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe unachafua hali ya hewa lakini wao wanazalisha umeme kwa kutumia makaa hayo kwa sababu teknolojia imebadilika,” amesema.
“Duniani kote umeme wa bei nafuu ni unaozalishwa na maji ama Makaa.”

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata