WANUFAIKA WA TASAF KAHAMA WAUPOKEA KWA MIKONO MIWILI MPANGO WA AWAMU YA TATU WA KUANZISHA VIKUNDI VYA KUWEKA AKIBA.


WANUFAIKA WA TASAF KATIKA KATA YA KILAGO WAKIWA KATIKA MKUTANO WA HADHARA WAKIPEWA MAELEKEZO KUHUSU MPANGO WA TASAF AWAMU YA TATU WA KUANZISHA VIKUNDI VYA KUWEKA AKIBA.

KAHAMA
WANUFAIKA wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) katika halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga wamesema kuwa mpango wa awamu wa tatu wa kuanzisha vikundi vya kuweka pesa utawasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato cha familia na kuondokana na utegemezi.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ufala kata ya Kilago wilayani Kahama baadhi ya wanufaika wa mpango wa TASAF wamesema kuwa vikundi vitawasaidia kubadilishana uzoefu ikiwa pamoja na kufanya kazi za ujasiliamali kwa ushirikiano.

Sambamba na hayo wameiomba Serikali kuwapatia elimu zaidi ya namna ya kuunda vikundi bora na kuanzisha miradi kwani wengi wao hawajui kusoma na kuandika na kwamba wakiwaacha wafanye peke yao hawatakuwa na vikundi vyenye tija.

Akijibu ombi hilo mratibu wa Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) Mkoa wa Shinyanga Dioniz Gastav amesema kuwa wametoa mafunzo ya siku tano kwa maafisa maendeleo wapatao arobaini hivyo watazunguka na kuwafikia walengwa hao kwa lengo la kuwapa elimu za uundaji wa vikundi katika halmashauri za Mbogwe na Kahama mjini.

Mfuko wa maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa sasa upo katika mpango wa mradi wa tatu wa kuziwezesha kaya masikini kuunda vikundi vya kuweka akiba na kuanzisha shughuli za kiuchumi ili kujionezea kipato.


SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata