NDUGU WAGOMA KUZIKA WAKIDAI MAREHEMU KANYOFOLEWA FIGO


Ndugu wa msichana Mahija Zahoro(16) wameahirisha mazishi wakidai kwamba mwili wa ndugu yao huyo umetolewa figo.
Ndugu hao wamelazimika kuacha kaburi wazi wakidai kwamba wamebaini michubuko kwenye mwili wa mtoto wao huyo huku wakibaini haukuwa na figo.
Akizungumzia mkasa huo leo baba mkubwa wa marehemu Selemani Simbambili mkazi wa Kwankonje Handeni alisema tarehe sita usiku, walipata taarifa ya kifo cha mtoto wao ambaye alikuwa Dar es Salaam akiwa mfanyakazi wa ndani aliyepoteza maisha ghafla akiwa usingizini.
Amesema siku ya pili walifanya taratibu za kuchukua mwili wa marehemu lakini walikuta hakuna taratibu zozote zilizofanyika kuripoti tukio hilo katika vyombo vya dola hali ambayo ilileta kutoelewana baina yao na tajiri aliyekuwa akiishi na mtoto wao.
Amesema hawakutaka malumbano zaidi walichukua mwili hadi Handeni ambapo siku ya pili waliamua kutozika na kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi Handeni na mwili ukafanyiwa uchunguzi hospitali.
“Tuliamua tusizike kwasababu ni kwanini wenzetu (mwajiri) hawakwenda kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola wakati amepata tatizo, lakini mwili una makovu kama mtu aliyeungua, huku wengine wakisema amechanwa ubavuni na kuhisi ametolewa figo ikabidi tuwe na wasiwasi”alisema Simbambili.
Mama wa marehemu Zawadi Daudi alikiri kuwa alivyokagua mwili wa mtoto wake alibaini una lengelenge kama mtu aliyeungua huku akitoka damu na povu mdomoni.
Mwenyekiti wa kijiji cha Palagwe kata ya Kwankonje Hamisi Yahaya alisema alipopokea taarifa kuhusu tukio hilo alikubaliana na familia waende polisi kwa uchunguzi zaidi ili kujiridhisha wote kwa pamoja.
Daud Felix ndugu wa mwajiri wa binti aliyefariki alisema hawajafanya chochote juu ya kifo cha Mahija kwani usiku wa tukio walikula naye chakula kama kawaida huku wakiongea na wenzake na wakaagana kwenda kulala.
Amesema asubuhi kuna mtoto wa tajiri wake alikwenda kumuamsha lakini hakuamka ndipo wakastuka kwanini haamki na kupelekwa hospitali ambapo daktari aliwaambia kuwa amefariki.
Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema taarifa za daktari zinaeleza kuwa mwili wa marehemu haujaonekana kuchanwa wala kupasuliwa popote na alama alizokuwa nazo ni za kawaida kwa mtu aliyefariki na ndani ya zaidi masaa24 akawa hajapatiwa huduma yoyote.
Amesema ripoti inaonyesha ni kifo cha kawaida na mwili kuwa na malengelenge ni kwa kuwa haujawekwa dawa tangu afariki na kusafirishwa hali hiyo ndio husababisha mabadiliko kwa mtu aliyefariki.
Baada ya ripoti ya daktari kubainisha kuwa marehemu hakufanyiwa jambo lolote katika mwili wake ndugu wa marehemu na wale waliokuwa wakituhumiwa walikubaliana na kwenda kuzika ikiwa ni siku mbili tangu kufariki kwake.
Na Rajabu Athumani,Mwananchi

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata