MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA,AWATAKA MAAFISA MAENDELEO KUFANYA KAZI NA SIYO KUJALI POSHO ZA TASAF..

Maafisa maendeleo ya jamii ambao wamepatiwa mafunzo na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) juu ya kuunda vikundi vya kuweka akiba ili kuzisaidia kaya masikini wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kujituma huku wakitambua ni miongoni mwa majukumu yao na siyo kazi ya Mfuko huo.

Wito huo umetolewa leo mjini Kahama na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, ANDERSON MSUMBA mwishoni mwa mafunzo ya siku tano kwa maafisa maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Mbogwe mkoani Geita na Kahama Mjini, mkoani Shinyanga.

MSUMBA amesema moja ya jukumu la Maafisa Maendeleo ya Jamii ni kuhamasisha uundaji wa vikundi vya ujasiriamali katika jamii na kwamba inachokifanya TASAF ni kuwaongezea ujuzi katika majukumu yao na siyo kwamba wao wanaisaidia TASAF.

Katika hatua nyingine, MSUMBA amewataka Maafisa hao wa Maendeleo ya Jamii kuweka mbele kazi na kupanga njia bora ya kuzifikia kaya masikini na siyo kuangalia posho wanazopata katika semina na kusahau majukumu yao katika jamii.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF mkoa wa Shinyanga, DIONIZ DASTAV amewataka maafisa hao kuyatumia vizuri mafunzo waliyopata ili kufanikisha uundaji vikundi kwa kaya masikini ili ziweze kujiongezea kipato.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa watawafikia walengwa na kuwapa elimu waliyopata pamoja na kuwasaidia kuunda vikundi na kuibua shughuli za miradi ya maendeleo.

Mafunzo hayo ya Siku tano ambayo yamewahusisha maafisa maendeleo ya jamii 40 kutoka halmashauri za Mbogwe na Kahama  mji yametolewa kupitia mpango wa TASAF awamu ya tatu unaolenga Kuunda vikundi vya kuweka akiba na kuanzisha shughuli za kiuchumi kwa kaya masikini.


 MATUKIO KATIKA PICHA:

MAAFISA MAENDELEO WA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA NA MBOGWE WAKIWA KATIKA SIKU YA MWISHO YA MAFUNZO YA SEMINA YA MPANGO WA TASAF AWAMU YA TATU.
 MAAFISA MAENDELEO WAKIWA KATIKA MWENDELEZO WA SEMINA HIYO
 


SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata