MAFURIKO KAHAMA:ZAIDI YA NG'OMBE 20 WASOMBWA NA MAJI USHETU.


 PICHA HII SI UHALISIA WA TUKIO
 KAHAMA
Zaidi ya ng’ombe ishirini wamesombwa na maji katika mto wa Mwabomba wakati wakijaribu kuvushwa kutoka halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama kwenda Masumbwe wilayani Mbogwe baada ya mto huo kujaa maji na kulifunika daraja katika barabara hiyo.

Tukio hilo limetokea jana mchana wakati ng’ombe hao waliokuwa wakivushwa na watu waliokuwa kwenye eneo hilo kwa ajili ya kazi ya kuvusha mizigo ya watu na mali zao walipozidiwa na mkondo wa maji na ng’ombe hao kusombwa na kupelekwa kusikojulikana. 

Awali wajumbe wa serikali ya kijiji cha Mwabomba wakiongozwa na JOHN MPANDUJI walitahadharisha juu ya hali ya usalama katika eneo hilo baada ya bidhaa za madukani zilizokuwa kwenye tela la trekta kusombwa na mafuriko hayo.

Kufuatia hali hiyo, wananchi wa kijiji cha Mwabomba wanakabiliwa na hali ngumu kiuchumi kutokana na shughuli zao nyingi kufanyika Masumbwe umbali wa kilometa 20 tofauti na Kahama ambako ni zaidi ya kilometa 100.

Diwani wa kata ya Mwabomba, YUDA MAJONJO amesema barabara hiyo iko kwenye mpango wa matengenezo na kwamba mafuriko hayo yatwasaidia wataalamu wa barabara kujionea hali halisi wakati wa kutathimini gharama za matengenezo yake.

Wakati madhara hayo yakijitokeza, NZALIA LUSAFISHA mmoja wa wamiliki wa mitumbwi inayovusha watu na mizigo yao amesema amekuwa akijipatia kati ya shilingi elfu sabini hadi laki moja kwa siku ingawa amesema haombei mto huo uendelee kufurika.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata