KOCHA MKUU WA SIMBA ATUMA SALAMU KWA YANGA

Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Pierre Lechantre ambaye CV yake imewafunika makocha wote walioko Bongo kwa sasa, ametoa angalizo kwamba wanatakiwa kuwa makini kwa siku 24 kuanzia leo Jumatano, kabla ya mechi ya watani wa jadi.

Simba inafahamu kwamba kipindi cha hapa kati kabla ya kucheza na Yanga, itakuwa na mechi nyingi za ligi kuliko wapinzani wao, hivyo wakiteleza tu, basi ubingwa wanaukosa.

Simba kwa sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 49, zikiwa ni tatu zaidi ya Yanga inayoshika nafasi ya pili.

Ratiba ya Simba kabla ya kucheza na Yanga Aprili 29, mwaka huu ipo hivi; Aprili 9, itacheza na Mtibwa Sugar, Aprili 12 dhidi ya Mbeya City na Aprili 16 dhidi ya Prisons.
Aprili 20, itacheza dhidi ya Lipuli, kabla ya kupambana na Yanga Aprili 29.

Wakati Simba ikiwa na ratiba hiyo ya mechi nne za ligi kuu kabla ya kucheza na Yanga, wenzao hao watacheza mechi moja tu ya ligi ndiyo mtifuano wa Aprili 29 ufike.

Yanga ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya mtoano, kwenye ligi kabla ya kucheza na Simba, itapambana na Singida United, mchezo utakaopigwa Aprili 11, mwaka huu.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, Aprili 7 itacheza na Wolaitta Dicha ya Ethiopia hapa nyumbani, kisha Aprili 18, itarudiana na timu hiyo huko ugenini.

“Tunatakiwa kupambana kweli kwani wenzetu watakuwa wakisubiri kuona tunateleza wapi ili wao wakija watuvuke, hatutaki kuona hilo linatutokea, hivyo vijana wangu lazima watambue kwamba tupo kwenye mapambano makali katika kuelekea kutimiza malengo yetu ya kuwa mabingwa,” alisema Lechantre.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata