AUWAWA KWA KOSA LA KUTAPELI MBUZI

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mateso Milu Bujingi (35) ameuwawa na kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kumpiga mawe na fimbo sehemu mbali mbali za mwili wake kwa kosa la kutapeli mbuzi wawili wenye thamani ya shilingi elfu 55

Hayo yamebainishwa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi Ahmed Msangi na kusema mbali na mtu huyo kuuwawa, Polisi walifanikiwa kumuokoa Malecha Gilala (38) ambaye naye alikuwa anashirikiliana na marehemu kufanya utapeli huo nyumbani kwa bwana Lubeja Tulu, kwa kujifanya wao ni maofisa wa Polisi kuwa wamekwenda kwake kwa lengo la kumkamata kutokana na mgogoro wa shamba uliopo kati yake na jirani yake na kutaka wapatiwe kiasi cha fedha laki mbili ili wasiweze kumpeleka Polisi.

Aidha, Kamanda Msangi amesema tukio hilo limetokea jana (Aprili 04, 2018) majira ya saa 11:30 jioni katika kijiji cha Nyanzumula kata ya Kagunga tarafa ya Nyanchenche wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

Inadaiwa kuwa kutokana na Lubeja kutokuwa na fedha hizo aliwapa mbuzi wawili vijana hao ili wasiweze kumkamata lakini kwa bahati mbaya matapeli hao walirudi siku nyingine wakitaka wapatiwe tena ndipo Lubeja alipoamua kuenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa pamoja na Polisi lakini wakati askari walipokuwa wanafanya ufuatiliaji wa kwenda eneo la tukio ghafla wananchi wenye hasira kali waliwavamia na kuanza kuwashambulia matapeli hao na kupelekea mmoja kufariki wakati alipokuwa akikimbizwa hospitalini kutokana na kipigo alichokipata.

Kamanda Msangi amesema mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa kukamatwa kuhusiana na tukio hilo, huku akitoa onyo kwa wananchi kuacha tabia ya kutumia majina ya vyombo vya ulinzi na usalama katika kufanya uhalifu.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata