WAJAWAZITO WAPIMIWA AFYA ZAO KWENYE VYUMBA VYA MADARASA


Morogoro. Wananchi wa Kijiji cha Dakawa- Ukutu mkoani Morogoro wamelalamika kutumia vyumba vya madarasa kupimiwa afya zao, wakiwamo wajawazito.

Wananchi hao wanasema wanalazimika kutumia madarasa ya Shule ya Msingi Dakawa kwa sababu ya kukosekana hospitali ya karibu.

Kwa mujibu wa wananchi hao kila wanapotumia madarasa walimu wanalazimika kuwatoa watoto ndani na hii ni kila mwisho wa mwezi ili watoto na wajawazito wapatiwe matibabu. “Wajawazito tunapimwa kwenye madarasa ya wanafunzi, watoke nje sisi ndio tunaingia darasani tunalazwa chini tupimwe, kwa kweli hii inatuumiza sana,” alisema mjazimto aliyejitaja kwa jina moja la Mwajuma.

Umbali wa kutoka kijijini hapo hadi kituo cha afya ni kilomita 25, jambo wanalodai linasababisha wanawake wengi kujifungulia njiani kabla ya kufika hospitalini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanakijiji hao wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasogezea huduma hiyo karibu ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto. Naye Mwajuma Malozo alisema changamoto ya huduma hizo inawaumiza zaidi wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano ambao huhitaji huduma hizo mara kwa mara.

“Changamoto kubwa hapa ni huduma za afya hatuna, pindi Serikali inaposema inafanya jambo kijiji hiki kinarukwa hatujui kwa nini, tunashindwa kupiga hatua kuna jengo la zahanati wanakijiji tumejenga lakini linazidi kuchakaa tunaambiwa itafunguliwa lakini mpaka leo kimya,” alisema Chaurembo ambaye pia ni Imamu wa Msikiti wa Dakawa.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hassan Mwanda alisema, “kwetu tunaona ni kashfa mama anapojifungulia njiani na watoto wanamuona, sasa hivi tuna changamoto ya magonjwa ya kuhara watoto na hata watu wazima kufuata huduma mbali na hakuna usafiri inafikirisha. Tumejitahidi tumejenga kituo basi tunamuomba waziri wa afya aliangalie ili alete wataalamu kifunguliwe,” alisema Mwanga.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Duthumi ambacho ndiyo tegemezi la wakazi wa Dakawa – Ukutu, Dk Kazimili Subi alisema changamoto ni umbali wa baadhi ya vijiji ambavyo havina zahanati na vimesalia kuitegemea Duthumi.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata