RAIS MAGUFULI AKOSHWA NA UTENDAJI WA KIWANDA CHA NDEGESELA MJINI KAHAMA,AWATAKA WAFANYABIASHARA WENGINE KUACHA UJANJA UJANJA.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Magufuli,amewataka baadhi ya Wafanyabiashara kuacha biashara za ujanjaujanja kwa lengo la kukwepa kodi pindi wanapoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.
Rai hiyo aliitoa jana mjini Kahama,wakati wa ziara yake ya siku mbili wilayani Kahama,katika Kiwanda cha Kahama oil Mill,alichokitembelea na kuelezwa changamoto nyingi zinazokwamisha uendeshaji wa viwanda kwa wazawa.
Katika kiwanda hicho Rais Magufuli,alisema Wafanyabiashara hao wamekuwa wakitumia ulaghai pindi wanapoagiza bidhaa toka nje ya nchi kwa kutumia hila kuwa walichoagiza ni malighafi na kutozwa ushuru mdogo kumbe ni bidhaa kamili inayokwenda moja kwa moja kwenye masoko.
Aidha Magufuli alisema wafanyabiashara wakiishatoa mizigo hiyo bandarini kwa ushuru mdogo,wanaweka kwenye vifungashio na kuingia sokoni kwa kuuza bei ya chini hali inayoathiri masoko ya bidhaa zinazotengenezwa na viwanda vya ndani.
Kufuatia hali hiyo aliziagiza mamlaka husika kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo kwa kuwatoza ushuru mkubwa wafanyabiashara wanaobainika kufanya hila hizo,huku akiviagiza vyombo vinavyohusika na ukusanyaji wa mapato (TRA ) kuangalia vizuri wawekezaji wa viwanda vya ndani.
Awali Mkurugenzi wa Kahama Oil Mill Ltd,Mhoja Nkwabi,alieleza changamoto kubwa inayowakabili ni juu ya kodi ya malighafi za bidhaa wanazotengeneza ikiwemo rangi ya kupaka mabati ambayo hutozwa kodi kama bidhaa inayojitemea.
Alifafanua kodi hizo husababisha gharama kubwa za uendeshaji hali ambayo huchangia kiwanda kushindwa kujiendesha na kukabiliana na ushindani wa soko la bidhaa kutoka nje ya nchi zenye gharama ndogo kwa watumiaji,hivyo kuomba serikali iangalie upya kanuni za bidhaa kutoka nje ya nchi ili kulinda bidhaa za ndani.
Alisema kampuni iliyoanzishwa mwaka 2002,ikimilikiwa na Wazawa kwa lengo la kukamua mafuta ya pamba na alizeti,lakini kutokana na uhaba wa malighafi wa mbegu za pamba ililazimika mnamo mwaka 2004 kuanzisha kiwanda cha kuchambua pamba,ili kuwawezesha kupata malighafi hiyo kwa urahisi.
Alibainisha mafanikio ya kampuni hiyo iliyowezeshwa na benki ya CRDB ni kuanzishwa kwa viwanda vya chuma kinachotengeza mabomba ya maji safi na taka na bati sambamba na kile  cha kutengeneza vyombo vya plastiki,huku ikiajiri wafanyakazi wa kudumu 120 na wa msimu 600 hivyo kusaidia ongezeko la ajira nchini.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata