NAIBU WAZIRI: CHUMVI, CHOKAA ZINAWEZA KUITAJIRISHA KIGOMA

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, amesema kwamba ikiwa wananchi wa Kigoma watatumia vyema fursa za upatikanaji wa Madini ya Chumvi na Chokaa, zilizopo katika Mkoa huo, wanaweza kutajirika.

Akihitimisha ziara yake katika Mkoa huo, jana Machi 3, baada ya kutembelea Migodi mbalimbali ya Madini ya Chokaa na Chumvi, Nyongo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa upatikanaji wa Chumvi na Chokaa ni neema kwa wananchi hao kutokana na uhitaji wake mkubwa katika maisha ya kila siku.

“Ni fursa kubwa sana kwa wananchi wa Kigoma. Wasidhani kwamba fursa iliyopo hapa ni ya uvuvi na mawese peke yake; wanaweza kuwa matajiri wakubwa kupitia Madini ya Chokaa na Chumvi.”

Akifafanua zaidi, Nyongo alisema kuwa, katika siku mbili za ziara yake mkoani Kigoma, ameshuhudia maeneo mengi yenye Chokaa ya kutosha na kwamba uzalishaji wake ni rahisi sana kwani kinachohitajika ni kuyachoma mawe husika na kusaga; basi.

Akizungumzia upande wa Chumvi, alisema kuwa, Mgodi wa kuzalisha Chumvi wa Nyanza, uliopo Uvinza unafanya kazi nzuri katika uzalishaji lakini kwa bahati mbaya asilimia 70 ya bidhaa wanayozalisha, huiuza nje ya nchi hususan katika nchi jirani za Kongo na Burundi.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata