MIKOA SITA KUANZA KUSAJILI LINE KWA VIDOLE

Dar es Salaam. Mikoa sita nchini imeanza kwa majaribio utekelezaji wa  mfumo wa kusajili laini za simu kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kielektroniki inayohusisha uchukuaji wa alama za vidole.

Akizungumza leo Alhamisi Machi 1, 2018 katika hafla fupi ya uzinduzi wa mfumo huo katika viwanja vya Mlimani City Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), Mhandisi James Kilaba ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Pwani, Iringa, Tanga, Singida na Zanzibar.

Amesema hatua hiyo imetokana na changamoto wanazokumbana nazo katika usimamiaji wa huduma hiyo, Amebainisha kuwa katika utumiaji wa simu za mkononi kumekuwa na udanganyifu katika kutoa taarifa za wanaosajili namba zao huku baadhi wakitumia simu kufanya uhalifu.

"Kutokana na changamaoto hizo na kuongezeka kwa watumiaji wa huduma hii kuna umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za watumiaji kwa ajili ya matumizi ya usimamizi, kiuchumi na kiusalama,” amesema.

Amesema mfumo huo pia utawezesha kupatikana takwimu kuhusu watumiaji wa simu za mkononi kwa ajili ya kuweka mipango ya kuendeleza sekta ya mawasiliano.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata