BANK YA CRDB KUTOA MIKOPO HADI SHILINGI MILIONI 50 BILA RIBA.

BENKI ya CRDB inatoa mikopo ya hadi Sh. milioni 50, isiyo na riba ndani ya siku 50 za kwanza, kwa wateja wake wenye kadi zake mpya za kutolea fedha za Mastercard Gold Credit na Mastercard World Reward.

Akizungumza na Nipashe iliyotaka kupata ufafanuzi juu ya huduma hiyo jana, Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa CRDB, Tuli Mwambapa, alisema kiwango cha chini cha mikopo hiyo ni Sh. 500,000 na cha juu ni Sh. milioni 50.

"Kiwango cha juu ni Sh. milioni 20 kwa Mastercard Gold Credit (wateja wa kawaida) na kwa wale wenye kadi za Mastercard World Reward (wateja wakubwa) ni Sh. milioni 50," alisema.

Mkurugenzi huyo alisema mikopo kwa wateja wote wenye Mastercard Gold Credit itatolewa bila riba kwa siku 45 za mwanzo wakati kwa wateja wenye Mastercard World Reward itatolewa bila riba kwa siku 50 za kwanza.Mwambapa alisema huduma hiyo ilianza kutolewa rasmi na CRDB Februari 21.

Hata hivyo, kwa kipindi kinachozidi siku hizo kabla ya mkopo kumalizika kurejeshwa mteja atatozwa riba ya asilimia tano, alisema Mwambapa.

Mama Mwambapa alitaja sifa za kupata kadi hizo kuwa ni mteja wa CRDB anayelipwa mshahara kupitia benki hiyo.

"Sifa nyingine ni wateja ambao kampuni zao zina mkataba wa makubaliano na CRDB kuhusu mikopo binafsi, na wateja wenye vikundi vya wajasiriamali wadogo na wa kati na kampuni kubwa ambazo zina ubia na CRDB," alisema.

Mkurugenzi huyo pia alisema ili mteja apate mkopo, anatakiwa ajaze fomu ya maombi ambayo yatafanyiwa tathmini kwa taratibu za benki kupitia idara ya mikopo.

Alisema mteja atakayekidhi vigezo atapewa mkopo na anaweza kutoa fedha kupitia kadi yake ya ATM au kwa kufanya muamala kwa njia ya mtandao.

"Katika kiasi anachopewa mteja kama mkopo, asilimia 30 anaweza kuchukua fedha taslimu kupitia ATM wakati asilimia 70 anatakiwa kutumia mashine maalum za malipo."

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata