VIBANDAUMIZA VYASABABISHA WANAFUNZI WANNE KUKATIZA MASOMO YAO


Mtwara. Wanafunzi wanne wa Shule ya Msingi Nalingu  wilayani Mtwara, wamekatiza masomo kutokana na kupata ujauzito.

Mabanda ya kuonyesha picha na mpira maarufu vibanda umiza, watoto kutoridhika na hali za maisha ya wazazi/walezi na malezi duni vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu za wao kupata ujauzito.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumatatu Februari 19,2018, mmoja wa wanafunzi hao, Maria (16) ambaye sasa ni mama wa mtoto wa miezi miwili anasema alipata ujauzito mwaka jana akiwa na umri wa miaka 15 alipoanza uhusiano na kijana mmoja lakini kwa sasa hajulikani alipo.

“Ilitokea bahati mbaya kupata mimba, nilikuwa sijui kama ninayofanya ni kosa kwa sababu mara kwa mara mimi na baba wa mtoto wangu tulikuwa tukienda kuangalia video (picha) usiku, baada ya kumtoroka mama yangu na kufanya yaliyosababisha nikatize masomo,”anasema Maria.

Mwathirika mwingine, Happiness aliyepata mimba akiwa darasa la saba na miaka 16, anasema aliingia katika uhusiano wa mapenzi baada ya kurubuniwa na kijana aliyemuahidi kumpa Sh7,000 wakati akielekea sokoni na kulazimika kuungana naye kwenda mabanda ya video siku zilizofuata.

“Kwa sasa sina wa kumwachia mtoto ninalazimika kwenda naye katika vibarua ili nipate fedha ya kumhudumia kwa sababu mama yangu ni mgonjwa, nalazimika kumhudumia,” amesema Hapiness.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Riziki Mwilombe anasema chanzo cha tatizo hilo ni malezi mabovu kwa baadhi yao kwani wengi wao hupata fursa za kutembea usiku na wengi wanalelewa na mama pekee.

“Mwaka 2017, nilikuwa na tatizo la mimba kwa wanafunzi watatu, wawili wa darasa la saba na mmoja darasa la sita, sehemu kubwa imesababishwa na uwapo wa fursa za kutembea usiku hususan kwenye mabanda ya sinema ambako ndiko chanzo kikubwa cha baadhi yao  kupata ujauzito,”amesema mwalimu Mwilombe.

Kaimu mtendaji wa kijiji cha Nalingu, Amosi Byabato anasema kuhusu mabanda ya kuonyesha picha tayari mkuu wa wilaya ameshatoa maagizo.

Amesema kupitia sheria ndogo za vijiji, mabanda hayo hayaruhusiwi kufanya kazi mchana na nyakati za usiku hayaruhusiwi kuingiza mwanafunzi.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata