KIJANA AFARIKI KWA KUGONGWA NA TRENI, AKATIKA VIPANDE VIWILI

Eneo la tukio.

INATISHA! Kijana mmoja maarufu kwa jina la Sharobaro mjini hapa, aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20, ameuchapa usingizi chini ya daraja la reli kisha kupoteza maisha baada ya kukatwa vipande viwili na treni.

Tukio hilo ambalo Ijumaa Wikienda lilifika punde baada ya kujiri, lilitokea kwenye daraja lililopo Barabara ya lringa- Morogoro, eneo la Msamvu, mchana wa Ijumaa iliyopita na kuibua masikitiko makubwa.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, wasamaria wema waliishuhudia maiti ya kijana huyo ikiwa imekatwa vipande viwili ndipo wakatoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya mtaa huo ambao nao ulitoa taarifa polisi.

Akilisimulia Ijumaa Wikienda juu ya tukio hilo la kutisha, mmoja wa mashuhuda hao, Mohamed Shukuru alikuwa na haya ya kusema:

“Kama unavyoona, chini ya daraja hili kuna reli na kunapita treni na juu yanapita magari kuelekea mkoani lringa.

“Sasa baadhi ya watu wa Stendi ya Msamvu hupenda kupumzika chini ya daraja hili na wengine hulala hapahapa.

“Kwa hiyo kinachoonekana, huyu jamaa alipitiwa na usingizi. Sasa treni ilipofika hakuisikia na kujikuta akigongwa kisha kupoteza maisha. Kiukweli ni tukio la kutisha sana.”

Shuhuda mwingine, Jumanne ldd alisema: “Huenda watu wamemuua na kuja kumtupa hapa relini kwa lengo la kupoteza ushahidi. Haiingii akilini, hata uwe chizi kiasi gani, huwezi kuja kulala relini. Vilevile hata ulewe vipi, mgurumo wa treni ni mkubwa hivyo lazima angeamka, binafsi siamini kama huyu kijana amegongwa na treni. “Hebu wahusika wafanye uchunguzi wao kwa kina ili tujue ukweli wa hili tukio.

Ijumaa Wikienda liliwashuhudia Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wa Mkoa wa Morogoro wakiwa bize kupima eneo la tukio na baada ya kumaliza kazi hiyo waliuchukua mwili wa marehemu huyo na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kusubiria kama kuna ndugu watajitokeza kwani hakukuwa na yeyote aliyemtambua kwenye eneo hilo la tukio.

Credit: Global Publisher

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata