AGIZO LA MKUU WA MKOA WA GEITA LADAIWA KUPUUZWA


Pamoja na mkuu wa mkoa wa Geita mhandisi Robert Gabriel kufika katika eneo la tukio la machimbo ya dhahabu ya Nyakafuru wilayani Mbogwe na kushuhudia wachimbaji wadogo wakilalamikia kikundi cha Isanjabadugu kinavyowapora mawe yenye madini wachimbaji hao, hali ambayo RC huyo ilimfanya kuagiza serikali wilayani humo pamoja na ofisi ya madini ya mkoa kumaliza tatizo hilo lakini agizo hilo limeonesha kupuuzwa.
Katika ziara yake mhandisi Gabriel alionyesha kukerwa na tabia ya unyanyasaji kwa wachimbaji wadogo wa machimbo hayo ingawa pamoja na kumpata afisa madini afafanue lakini ufafanuzi wake haukumridhisha mkuu huyo wa mkoa baada ya kuelezwa namna kikundi cha Isanjabadugu kinavyowanyanganya mawe na kuwatoa kwenye machimbo wanayopata dhahabu kwa kisingizio wao ndiyo wasimamizi walioteuliwa na serikali.
Juzi afisa madini mkazi wa mkoa wa Geita Ally Said alisema tayari Jumatatu iliyopita alituma wataalamu wake kwenda kwenye machimbo hayo kumaliza mgogoro huo lakini hadi kufikia jana kikundi hicho bado kinaendelea kukusanya mawe asilimia 30 ya kila shimo hali ambayo wachimbaji hao waliilalamikia mbele ya mkuu wa Mkoa huyo kwamba kikundi hicho hakijawekeza rasilimali yoyote kwenye machimbo hayo lakini kimekuwa kikichukua mawe mifuko 30 kwa kila shimo lenye mifuko 100.
Sabuni Jasaga ni mchimbaji anayemiliki shimo katika machimbo hayo ambaye alisema kikundi hicho ni kama madalali wanaotumiwa na wakubwa kwa kuwakusanyia pesa kwani wanaelewa kabisa Isanjabadugu hana eneo wala hatumii gharama yoyote kwenye uchimbaji lakini ndiye anayechukua mawe mengi kwa kisingizio cha usimamizi wa shughuli za uchimbaji.
“Ndugu mwandishi watu hawa wana pesa nyingi sana wamehonga kuanzia wilaya hadi mkoa hivyo hata kama tungelalamikaje kikundi hicho kinakusanya mawe kwa ajili ya wakubwa, hata wao wenyewe wanadai wako kwenye mgongo wa viongozi wakubwa wa serikali haiwezekani waruhusiwe kuvuna mawe yote hayo wakati anayefanya kazi ni mchimbaji ambaye ndiye huteseka kupasua miamba lakini mawe yanapopatikana tayari isanjabadugu hufika na kuchukua mgawo wao bila kazi yoyote huo ni unyonyaji”, alisema Jasaga.
Pamoja na hali hiyo mmiliki mwingine wa shamba katika eneo hilo Daud Mabenga alisema walishaandika barua sehemu mbalimbali za serikali lakini hakuna majibu hata wenyewe wenye mashamba kikundi hicho kikishachukua mifuko 30 bure huwapa mifuko mitano tu huku 25 iliyobaki kudai ni mali ya wakubwa ngazi ya Wilaya na Mkoa mbaya zaidi shimo hadi kulifikisha kwenye mawe kazi hiyo hufanywa na zaidi ya watu 50 ambao huachiwa asilimia 70.
Mabenga alisema katika asilimia hizo 70 huingizwa kodi mbalimbali wakati mwingine kubaki na asilimia 40 ambayo hufanya waliopasuka mikono kupasua miamba ya mawe kuambulia mfuko 1 watu wawili huku idadi kubwa huchukuliwa na kikundi hicho ambao hawajui hata kushika nyundo kupasua miamba na kwa siku wanauwezo wa kuvuna bila jasho mifuko zaidi ya 300.
Aliomba serikali iwaondoe kama alivyoagiza mkuu wa mkoa wa Geita kumaliza tatizo hilo kwani kazi ya uchimbaji ni ngumu inapaswa kubaki wachimbaji na mashimo yao na kodi za serikali mambo ya mtu kati yaondolewe kwa kuwa kwa hapo Nyakafuru eneo hilo ni la mwekezaji sasa hicho kikundi hakina maana yoyote kuwa dalali wa kukusanya mawe ya wakubwa.
Alipotakiwa kuzungumzia hilo kamanda wa polisi mkoa wa Geita Mponjoli Mwabulambo ambaye askari wake wa kituo cha Wilaya ya Mbogwe wamekuwa wakituhumiwa kutumika kuwalinda na bunduki kikundi cha Isanjabadugu wakati wa kukusanya mawe hayo, alisema suala hilo linashughulikiwa na mkuu wa mkoa yeye hawezi kuliongelea kutokana na ngazi lilipo ni kubwa ni kubwa hivyo alidai Mkuu huyu alishatoa maelekezo ya kulimaliza.
Nae mkuu wa wilaya ya Mbogwe Martha Mkupas alipotakiwa kuzungumzia namna ya kikundi hicho kinachodaiwa kutumia pesa kuwahonga viongozi wote wa wilaya na Mkoa ili kiendelee kukusanya mawe hayo, alidai madai hayo ni ya uongo kwa kuwa wachimbaji wenyewe ndio waliochagua kisimamie shughuli zote za uchimbaji ingawa alisema kama wataendelea kulalamika na kuleta fujo atayafunga machimbo hayo kwa kuwa hayana mwenyewe eneo hilo ni la mtafiti wa kampuni ya Mabango.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikundi hicho Joseph Warwa aligoma kuzungumzia mgogoro huo licha ya mwandishi wa Blog hii kupiga kambi mjini Ushirombo kwa siku tatu lakini Warwa alikuwa akiahidia kukutana bila kuonekana hali ambayo mmoja wa viongozi wa kikundi hicho Evarist Gervas alisema kikundi hicho sio kwamba kimetokea Geita bali ni muungano wa wachimbaji kutoka Geita, Mbogwe na Bukombe ingawa hakuzungumzia tuhuma za kujipatia bure mawe yanayochimbwa na wachimbaji kwa kusimamiwa na serikali.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata