ZAIDI YA WATU 30 WAMELAZWA KAHAMA BAADA YA KULA UGALI WA KIPORO NA MBOGA ZA MAJANI MSIBANI.Zaidi ya watu 30 wa Kitongoji cha Isumbi kijiji cha Igung’hwa Kata ya Kinaga Wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamelazwa katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Kahama baada  ya kudaiwa kula ugali wa Kiporo na mboga za majani wakiwa msibani.

Afisa Mtendaji wa kata ya Kinaga Paul Damasi amesema kuwa wananchi waliolazwa katika Hospitali ya mji wa Kahama ni wale waliokula chakula cha  ugali wa kiporo na mboga za majani aina ya mgagani.

Damasi ameyasema hayo jana wakati akiongea na wananchi Kijiji cha Igung’hwa waliohudhulia msiba huo uliotokea nyumbani kwa Salum Manyanda na kuongeza kuwa asilimia kubwa ya watu waliougua ghafla baada ya kula chakula hicho ni wanawake.

Afisa mtendaji huyo wa Kata amesema kuwa tukio hilo la aina yake limetokea jana majira ya saa tano asubuhi baada ya waombolezaji kula chakula kilichobakia jana yake huku akieleza kuwa wagonjwa wote waliougua ghafla walikimbizwa katika hospitali ya Kahama kwaajili ya kupatiwa matibabu.

Naye Joyce samweli  akiongea na Kijukuu Blog wakati wakipeleka chakula msibani jana alikutana na wakina mama wenzake waliougua ghafla ugonjwa huo wakipakizwa kwenye magari ya kubebea wagonjwa wakati huo wengine wakicheka cheka na wengine wakidai wanakosa nguvu.

Naye mwananchi mwingine Michael simon mkazi wa Kahama mjini amewashauri viongozi wa kijiji hicho kuondokana na dhana ya kupeleka vyakula misibani badala yake wanapaswa kupika chakula hicho wakiwa katika eneo husika la msiba.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Igung’hwa William Katwiga akizungumza na mwandishi wa habari hizi amesema kuwa ushauri huo wa  wananchi utazingatiawa na kudai kuwa wao kama wananzengo wamejifunza kutokana na makosa.

Naye mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Frederik Malunde amekiri kuwapokea wagonjwa hao na kusema kuwa waliowapokea walikuwa wanalalamika kuumwa kichwa,Tumbo,Kutapika na wengine kupoteza fahamu.

Sambamba na hayo Malunde amesema kuwa katika tatizo hilo kuna mambo mawili kwanza huenda ugali uliolala ulikuwa umeingiliwa na wadudu au mboga za majani walizochuma zilichanganyika na majani yasiyo chakula.

Dr malunde ameongeza kuwa kwasasa amebaki mgonjwa mmoja na wagonjwa wengine wameruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu.SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata