WAZIRI KAIRUKI AKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINAWAZIRI WA MADINI, ANGELLAH KAIRUKI (WA PILI KUTOKA KULIA) AKIJADILIANA JAMBO NA UJUMBE KUTOKA UBALOZI WA CHINA NCHINI ULIOONGOZWA NA BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA, WANG KE (KATIKATI).


 Na Mohamed Saif
 DAR ES SALAAM


Serikali imewakaribisha wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya madini nchini.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ametoa wito huo Novemba 16, 2017 Jijini Dar es Salaam alipokutana na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Wang Ke na ujumbe alioambatana nao Wizarani hapo kutoka kwenye Ubalozi huo ili kujadiliana masuala mbalimbali ya madini ikiwemo fursa za uwekezaji.

Waziri Kairuki alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini na hivyo zipo fursa lukuki za uwekezaji ambazo zinaweza kutumiwa na kampuni za nchini China kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Rasilimali za madini ni nyingi na hivyo zipo fursa mbalimbali ambazo zinaweza kutumiwa na kampuni za China na wakati huo huo kuchangia katika uchumi na pato la Taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki vile vile alisema yapo maeneo ambayo wawekezaji wanaweza kushirikiana na Serikali ambapo alitaja baadhi yake kuwa ni uchimbaji wa madini kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), tafiti za utambuzi wa maeneo yenye madini kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo cha Madini (MRI). 

Aidha, aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha madini yanayochimbwa nchini yanaongezwa thamani kabla hayajasafirishwa ili kukuza uchumi wa Taifa na wakati huo huo, kuongeza mapato ya Serikali na kuzalisha ajira zaidi.

“Madini yakiongezwa thamani hapa nchini, faida zitakazopatikana ni nyingi na ni kubwa ikiwemo ajira lakini pia mapato nayo yataongezeka kwa kuelewa thamani halisi ya madini husika,” alisema Waziri Kairuki.

Kwa upande wake Balozi Ke alipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuwaletea wananchi wake maendeleo endelevu.

Alisema Serikali ya China itaendeleza ushirikiano wa karibu na wa dhati na Serikali ya Tanzania hususan kwenye Sekta ya Madini ili kuhakikisha sekta hiyo inaleta tija iliyokusudiwa kwa Taifa.

Alisema kampuni mahiri nyingi kutoka China tayari zimeonyesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Madini na ziko tayari kuja kuwekeza Nchini. 


 MATUKIO KATIKA PICHA:

WAZIRI WA MADINI, ANGELLAH KAIRUKI (KULIA) AKIMSIKILIZA BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA, WANG KE ALIPOMTEMBELEA OFISINI KWAKE JIJINI DAR ES SALAAM ILI KUJADILI MASUALA MBALIMBALI.


 BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA, WANG KE (KULIA) AKIWA NA UJUMBE WAKE KUTOKA UBALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA WALIPOMTEMBELEA WAZIRI WA MADINI, ANGELLAH KAIRUKI (HAYUPO PICHANI) ILI KUJADILI MASUALA MBALIMBALI YA SEKTA YA MADINI.
 
WAZIRI WA MADINI, ANGELLAH KAIRUKI (WA PILI KUTOKA KULIA) AKIJADILIANA JAMBO NA UJUMBE KUTOKA UBALOZI WA CHINA NCHINI ULIOONGOZWA NA BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA, WANG KE (KATIKATI).WAZIRI WA MADINI, ANGELLAH KAIRUKI (KULIA) AKIJADILIANA JAMBO NA BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA, WANG KE.


SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata