WAKULIMA WA TUMBAKU KAHAMA WALIA NA TOZA ZA USHURU KWENYE MIKOPO YA KUNI.Wakulima wa Zao la Tumbaku katika Mkoa wa Kitumbaku Kahama wameiomba Halmashauri ya Ushetu kusitisha zoezi la kutoza ushuru kwenye mikopo ya Kuni inayotolewa na Taasisi za kifedha ili kuwapunguzia mizigo katika ulipaji wa madeni.

Ombi hilo limetolewa na Diwani wa Kata ya Bukomela KULWA SHOTO wakati akiwasilisha hoja binafsi katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Ushetu kilichoketi  Novemba 6 na 7  mwaka huu katika kata ya Nyamilangano.

Amesema wakulima wa Tumbaku mkoani humo hawajashirikishwa katika zoezi hilo hivyo ipo haja ya kupewa nafasi ya kuelezea changamoto wanazokabiliana nazo katika utayarishaji kuni za kuchomea Tumbaku.

Akijibu Hoja hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo MICHAEL MATOMORA amesema Ushuru wa kuni haukwepeki hivyo kila Mkulima wa Tumbaku atalazimika kulipia gharama hizo kwa mujibu wa sheria.

Amefafanua kuwa kumekuwepo kwa tatizo la wakulima kukwepa kulipa ushuru huo wakizani kuwa si wajibu wao jambo ambalo halmashauri hiyo haikubaliani nalo na kwamba watazidi kuchukua hatua za kisheria kwa  wanaokiuka utaratibu huo.

Zao la tumbaku ni miongoni mwa mazao ya biashara yanayoiingizia kodi kubwa Halmashauri ya Ushetu ambapo kwa mwaka huingiza  fedha zaidi ya shilingi bilioni moja.


SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata