MIILI YA WAPENZI YAKUTANA CHUMBA CHA KUHIFADHIA MAITI MBEYA NI TUKIO LA KUSIKITISHA

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Mohammed Mpinga.

Ni nadra kwa miili ya wapendanao kukutana katika nyumba ya kuhifadhia maiti baada ya wote wawili kuuawa, lakini hivyo ndivyo ilivyowakuta mwanaume aliyetambulika kama Musa Musa (42) na mwanamke aliyetajwa kuwa ni Salome wilayani hapa mkoani Mbeya.

Musa alikuwa akifanya kazi za ulinzi katika kata ya Itope aliuuawa kwa kipigo na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake Salome ambaye alifahamika kwa jina moja hilo, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Wakazi wa kata ya Makwale walisema Musa alimuua Salome baada ya kumfumania akiwa na mwanaume mwingine.

Akizungumza na Nipashe juzi, mwenyekiti wa kitongoji cha Itope, Emily Mwasongwe, alisema Musa alikuwa mlinzi wa nyumba na shamba vya mtu ambaye hakuweza kufahamika mara moja.

Mwasongwe alisema baada ya siku kadhaa tangu aanze kazi hiyo akitokea mkoa ambao haujafahamika, Musa alimpata Salome na wakawa wapenzi.

Alisema mwishoni mwa wiki iliyopita alipigiwa simu na watu kuwa mlinzi huyo amemuua mpenzi wake kwa kumchoma kisu tumboni baada ya kumkuta Salome akiwa na mwanaume mwingine.

Diwani wa kata hiyo, Thobias Mwamkonda alisema alipigiwa simu na mwenyekiti wa kitongozji hicho na kufika kweye eneo la tukio ambapo alipotoa taarifa polisi wilaya ambao walifika kuuchukua mwili wa marehemu.

Alisema polisi waliubeba mwili huo na kuupeleka hospitali ya wilaya ambapo uliwekwa chumba cha kuhifadhia maiti.

Lakini wakati serikali ya kata ikiwa hospitalini hapo, alisema zaidi Mwamkonda, walipata taarifa kuwa wananchi wamemkamata mtuhumiwa wa mauaji ya Salome kwenye kitongoji cha Kilambo, karibu na chem chem ya maji ya moto, wakati akijaribu kutoroka.

Mwamkonda alisema walipofika mahali hapo walikuta Musa ameshauawa kwa kupigwa na watu wenye hasira kali ambao walitokomea baada ya kufanya mauaji hayo.

Alisema Jeshi la Polisi lilibeba mwili huo na kuupeleka hospitali ya wilaya ya Kyela ambako ulihifadhiwa kwenye chumba cha maiti kile kile kilichokuwa na mwili wa Salome.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya, Dk. Francis Mhagama alithibitisha kupokea miili hiyo miwili.

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Mohammed Mpinga amekiri kuwepo na tukio hilo na kusema hakuna mtu aliyakamatwa akihusishwa na mauaji hayo. Kamanda mpinga aliwaasa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata