LUGOLA ACHIMBA MKWARA BULYANHULU,AWAPA SIKU 14 MGODI KUONDOA TAKA NGUMU LA SIVYO WATAUFUNGIA.

Serikali imetoa muda wa wiki mbili kwa Mgodi wa Acacia Bulyahulu kuziondoa taka ngumu Wanazozizalisha katika Mgodi huo hali ambayo inahatarisha usalama wa Mazingira.

Kauli hiyo imetolewa  na Naibu Waziri  wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira KANGI LUGOLA alipotembelea Mgodi huo kujionea hali ya Mazingira na usalama mahala pa kazi.

Amesema serikali haitakubali kuona taka hizo zinaendelea kurundikwa katika Mgodi huo, hali ambayo inaharibu mazingira na afya za Watumishi kwa kigezo cha kukosa mzabuni wa kuziondoa taka hizo zinazokadiriwa kufikia tani 200.

Naye Mratibu wa Baraza la Taifa la hifadhi ya Mazingira (NEMC) kanda ya Ziwa JAMAL BARUTI amesema Taka hizo zinapaswa kuondoshwa haraka na endapo watakaidi Agizo hilo watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria ya Mazingira.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mgodi huo ELIAS KASITILA amekiri kuwepo kwa taka hizo na kusema kuwa mzabuni aliyekuwa anaziondoa taka hizo mkataba wake umeshaisha na hivi sasa wanaendelea na mchakato wa kumtafuta mzabuni mpya.

KASITILA amefafanua kuwa Mgodi huo utatekeleza agizo hilo na kuiomba serikali kuharakisha uhakiki wa vibali vya kampuni zilizoomba zabuni hiyo ili zoezi la kuziondosha taka hizo liweze kufanyika.

Naibu waziri LUGOLA alikuwa na Ziara ya kikakazi ya siku Moja mjini Kahama na ametembea Halmashauri ya Msalala na Mji wa Kahama na ameahidi kuyafuatilia maangizo mbalimbali aliyoyatoa baada ya wiki mbili kukamilika.

MATUKIO KATIKA PICHASAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata