CCM WALIA KUFANYIWA FUJO NA UPINZANI K'NJARO

Wakati kampeni za udiwani zikiendelea katika maeneo mbalimbali nchini, Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro kimedai kufanyiwa fujo na wafuasi wa upinzani pindi wafuasi wao wanapomaliza mikutano yao.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Katibu wa chama hicho mkoani hapa, Jonathan Mabihya katika mkutano wa kampeni za marudio ya uchaguzi wa udiwani Kata ya Bomambuzi.

Mabihya aliliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua za kisheria wafuasi hao wa upinzani, huku akiwasisitiza wanachama wa CCM kutowajibu kwa fujo.

Katibu huyo aliwataka wanachama wote wanaoshiriki kwenye kampeni kufanya siasa safi na kunadi sera za chama hicho kwa kuzingatia sheria ikiwamo kufuata kanuni.

Pia, Mabihya aliwataka wananchi wa Kata ya Bomambuzi kutokubali kudanganywa kwa kilo moja ya nyama na sukari wanazopewa na wapinzani ili kuuza kura zao, badala yake wafanye uamuzi sahihi wa kuchagua kiongozi atakayewatumikia.

Pia, katibu huyo aliliomba jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro kuingilia kati suala hilo akidai limekuwa likiwafifisha wafuasi wa chama hicho kushiriki katika mikutano yao kwa kuhofia kufanyiwa fujo.

Katibu msaidizi wa oganizesheni ya chama hicho, Steven Kazidi aliwataka wakazi wa Bomambuzi kutunza shahada zao za kupigia kura kwa ajili ya Novemba 26.

Aliwataka wananchi kutodanganyika na wapinzani kwa madai kwamba maendeleo yaliyopo wameyaleta.

“Wapo wanaopita majukwaani na kujitapa kuwa wao ndiyo wamewezesha maendeleo kwenye halmashauri zilizopo chini yao, ila si kweli, ukweli ni kwamba chama tawala ndicho kinachotoa fedha, kinatambua katika halmashauri kuna wananchi wao,” alisema Kazidi.

Aliwashauri wananchi kutokumchagua kiongozi kwa kuangalia fedha wala kabila bali wamchague mgombea wa CCM ili aweze kuwaletea maendeleo na kusimamia ilani ya uchaguzi inayoongoza dola.

Mgombea udiwani kupitia chama hicho, Juma Rahibu aliwataka vijana kutokubali kutumika na viongozi wa vyama vya siasa kwa lengo la kuhatarisha amani ya nchi.

Aliwashauri vijana kuungana ili kuhakikisha wanaleta maendeleo katika kata ya Bomambuzi.

Pia, aliwataka wakazi wa eneo hilo kuwa na msimamo katika shughuli za maendeleo huku akiahidi kuhakikisha anasimamia ilani ya uchaguzi pindi watakapompa ridhaa ya kuongoza.

“Mimi ni kijana mwenzenu, mkinichagua nitasimamia ilani ya chama changu pamoja na kuhakikisha asilimia tano zinazotengwa na halmashauri kwa ajili ya vijana zinawafikia vijana wote ndani ya kata hii,” alisema Rahibu.

Mwananchi.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata