WAZIRI AWAJIA JUU MAOFISA MAENDELEO WA JAMII

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewaibukia maofisa maendeleo ya jamii akiwataka kuwasilisha taarifa zitakazokuwa na idadi ya vikundi vya wanawake vinavyonufaika na mikopo pamoja na thamani yake.

Ummy aliyasema hayo mjini hapa juzi na kuonya kuwa ofisa atakayeshindwa kufanya hivyo kwa wakati atakula naye sahani moja ili iwe fundisho kwa watendaji wengine wasioweza kutimiza majukumu yao. Waziri huyo alitoa agizo hilo wakati akikabidhi msaada wa vitendea kazi kwa vijana 153 waliopatiwa mafunzo ya ujasirimali na utunzaji wa fedha kutoka Shirika la Brac Tanzania.

Alisema uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni kipaumbele cha Serikali lakini baadhi ya maofisa maendeleo ya jamii wameshindwa kusimamia bajeti ya asilimia tano kwa ajili ya mikopo kwa wanawake na vijana. Fedha hizo zinapaswa kutolewa na kila halmashauri nchini.

“Lazima nikiri kwamba maofisa maendeleo ya jamii wamechangia kwa kiasi kikubwa kutowezesha mpango wa uwezeshwaji wanawake kiuchumi katika ngazi ya halmashauri,” alisema.

Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Zena Said alisema kupitia shirika hilo vijana 153 wamepata fursa ya kujiajiri mkoani humo.

Ofisa Habari wa shirika hilo, Dotto Mnyadi alisema mradi wa kuwajengea uwezo na kupata fursa za kiuchumi kwa vijana umewanufaisha zaidi ya wasichana 700 ndani ya jiji hilo.

Alisema kuwa mradi huo uliwalenga zaidi vijana walio nje ya mfumo wa elimu kwa kuwajengea uwezo wa kusimamia fedha pamoja na mitaji yao.

Mwananchi:

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata