TUME YAKUBALI MASHARTI YA NASA

Nairobi, Kenya. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati ametangaza timu ya maofisa watakaosimamia shughuli za uchaguzi wa marudio Oktoba 26 huku jina la ofisa mtendaji mkuu, Ezra Chiloba likikosekana.

Chebukati, wakati anatangaza majukumu ya maofisa hao Ijumaa alisema Chiloba, ambaye muungano wa National Super Alliance (Nasa) unataka aondolewe, hatakuwa na mkono katika uchaguzi huo. Mbali ya Chiloba, pia maofisa wengine saba hawamo.

Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya maandamano makubwa kufanywa na wafuasi wa Nasa mjini Kisumu, Nairobi na Homabay wakishinikiza kuondolewa na Chiloba na wenzake 10.

Vilevile, mabadiliko hayo yamefanyika wakati Nasa wakitangaza kuongeza siku ya Jumatano katika siku za maandamano. Katika barua yao waliyopeleka polisi sasa Nasa watakuwa wakiandamana kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kushinikiza maofisa 11 waondolewe, na zifutwe zabuni kwa kampuni ya kuchapisha makaratasi ya kupigia kura na inayosambaza vifaa vya utambuzi wa mpigakura na kutuma matokeo kwa njia ya kielektroniki.

Baada ya shinikizo kali la maandamano ya ghasia, Chubukati ameonekana akikubali yaishe kwa upande wake akianza kwa kuondoa majina ya Chiloba na maofisa wengine saba.

Mabadiliko haya yanafanana na yale yaliyotangazwa siku chache baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta, lakini Tume ilikanusha.

Gazeti la The Nation limefahamishwa kwamba Chebukati alifanikiwa kuwashawishi makamishna wote na wakaridhia timu mpya ambayo itawajibika katika maandalizi na kujibu maswali yote yanayohusu uchaguzi wa marudio.

Timu mpya ni ya Marjan Hussein atakayekuwa msimamizi wa timu; David Towett atahusika na operesheni, Albert Gogo atasimamia teknolojia ya uchaguzi, Dk Sidney Namulungu atasimamia vituo vya kujumlishia kura, Tabitha Mutemi atasimamia mawasiliano, Agatha Wahome atahusika na fedha, manunuzi na utawala, na Salome Oyugi atahusika na masuala ya sheria.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata