DC MNYETI ASHINDA UJUMBE WA MKUTANO MKUU CCM TAIFA

Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Elexander Mnyeti leo amechaguliwa kuwa mmoja wa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM akiwakilisha wilaya ya kichama ya CCM ya Meru.

Mnyeti ambaye katika siku za karibuni, ameingia katika mgogoro na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akimtuhumu kuongoza njama za kuwanunua madiwani wa Chadema, alishinda baada ya kupata kura 266  akiwa hayupo ukumbini.

Katika nafasi hiyo ambayo ilikuwa inagombewa na wanaCCM 22, wajumbe wengine waliochaguliwa na Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha(AICC), Elishilia Kaaya  aliyepata kura 258 na  Dk Daniel Mirisho alipata kura 327.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, uliofanyika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Makumira, mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake wilaya ya Arusha, Mary Kisaka amesema  katika nafasi hiyo, waliopiga kura walikuwa 586 kura zilizoharibika zilikuwa 3 na kura halali 583.

Katika nafasi ya  Mwenyekiti wa CCM Wilaya Meru, mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Andew Mungure aliweza kutetea kiti hicho baada ya kuwabwaga wagombea wenzake wawili.

Mungure alipata kura 471 na kuwabwaga Nevangirwa Mmari aliyepata kura 106 na Daniel Kaaya aliyepata kura 28.

Katika uchaguzi huo, Mbwana Hungura alichaguliwa kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa wilaya hiyo baada ya kupata kura 50 na kuwashinda wanaCCM wengine wane ambapo kura halali zilikuwa ni 97.

Mwananchi:

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata