HALI TETE KWA WACHIMBAJI WADOGO MWIME KAHAMA,WAJISAIDIA VICHAKANI KWA KUKOSA VYOO.Hali ya maisha ya wachimbaji wadogo wa Mwime katika halmashauri ya mji wa Kahama bado ni tete pamoja na halmashauri kutoa siku 14 kwa wenye mashamba kuchimba vyoo lakini wachimbaji hao bado wanajisaidia vichakani hali ambayo inaweza kuhatalisha maisha yao kutokana na magonjwa ya mlipuko.


Mkuu wa idara ya afya na mazingira katika halmashauri ya mji wa Kahama Martine Masele alisema baada ya kufika eneo la machimbo hayo walibaini hali mbaya ya mazingira ya kujisaidia haja kubwa pamoja na uandaaji wa vyakula kama vile nyama ambayo huchinja mifugo kwenye eneo hilo bila kuwa na maji salama ya kuoshea.

Awali mmoja wa wakurugenzi wa machimbo hayo Joseph Andrew alisema tayari wameanza mkakati wa kuyafukia mashimo yenye vinyesi ingawa pamoja na kuwepo kwa vyoo vya muda lakini wachimbaji hao ambao wako zaidi ya elfu 3 wanajisaidia vichakani nyakati za usiku na kufanya mazingira ya kufanya kazi hizo kuwa hatarishi.

Hata hivyo Masele alisema baada ya siku 14 za kwanza walizowapa kwa ajili ya kurebebisha vyoo hivyo hawakuweza kutekeleza hali ambayo ofisi yake ilitoa siku zingine 14 ambazo zitaisha wiki ijayo na wanaendelea na ufuatiliaji katika eneo hilo.

Mmoja wa wachimbaji katika eneo hilo William Zuberi alisema serikali inapaswa kuweka nguvu zaidi kwenye hali ya mazingira kabla ya mvua hazijaanza kunyesha kwa kuwa zikinyesha maji yote yatateremsha kinyesi kwenye maeneo ya makazi ya watu.

Kufuatia hali hiyo Mwananchi lilibahatika kumpata kwa simu naibu waziri wa ofisi ya makamo wa Rais Mazingira Luhaga Mpina ambaye alisema ataanza ziara ya ukaguzi wa mazingira katika maeneo yote ya mgodi ya wachimbaji wadogo ikiwemo na mgodi wa Mwime uliopo takribani kilometa 3 kutoka katikati ya mji wa Kahama.

Wachimbaji hao wadogo wanachimba kwa usimamizi wa wenye mashamba ambao hulipwa asilimia 3 ya uzalishaji huku asilimia 7 ikibaki kwa wachimbaji hali ambayo wenye mashamba wanapaswa kusimamia shughuli zote za mazingira katika eneo hilo.

Kwa upande wake afisa madini mkazi wa wilaya ya Kahama Tandu Jirabi alisema yeye yuko likizo ingawa alisema swala hilo linawahusu watu wa mazingira katika halmashauri ya mji ambao wanapaswa kuzungumzia hali ya usafi katika eneo hilo.


SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata