SHABIKI WA RAYON SPORTS ANUNULIWA NA AS KIGALI, APEWA NYUMBA NA MSHAHARA MNONO

 TIMU ya AS Kigali ya Rwanda, imemnunua shabiki maarufu wa mahasimu wao wa Jiji, Rayon Sports aitwaye Rwarutabura.

Na hayo yanatokea siku chache baada ya AS Kigali kuwachukulia Rayon kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Nshuti Dominique Savio aliyeondoka The Blues kuhamia kwa ‘Wana Mji’.

AS Kigali imejiimarisha kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Azam Rwanda kwa kumajili Savio aliyekuwa anachezea kwa wapinzani wao wa Jiji Kigali, Rayon Sports.

Baada ya pigo la uwanjani, mabingwa wa Ligi Kuu ya Azam Rwanda wamepata pigo la jukwaani pia, kufuatia Rwarutabura kuachana na The Blues kwenda kwa ‘Wana Mji’.

Rwarutabura ni shabiki mzoefu na maarufu hata Afrika Mashariki kutokana na staili za ushabiki wake na amedumu Rayon Sports kwa miaka mingi iliyopita, lakini sasa hivi ameamua kuvua rangi za bluu na nyeupe na kuvaa njano na kijani.

 Rwarutabura alisema kwamba yeye anaipenda Rayon Sports, lakini baada ya kupewa ofa nzuri na AS Kigali imebidi abadilishe maisha.

“Rayon Sports naipenda sana, tangu nikijua mambo ya soka ni Rayon Sports tu, lakini mambo yamebadilika kazi ni kazi. Ushabiki wangu nimeshajua unaweza kubadilisha maisha yangu na familia yangu ndiyo sababu inanifanya niachane na Rayon Sports kwa sababu AS Kigali itanilipa mshahara na imenunulia nyumba ina maana, nitaachana na kulipa kodi,”alisema Rwarutabura

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata