MLINGA AWATAJA MAWAZIRI WAONGO BUNGENI

Mbunge wa jimbo la Ulanga mkoani Morogoro, Goodluck Mlinga amefunguka na kuwataja baadhi ya mawaziri wa awamu ya tano na kusema ni waongo wamekuwa wakitoa majibu bungeni kuwaridhisha wabunge na spika lakini si watekelezaji ya kile wanachokisema.

Mlinga amesema hayo leo bungeni na kumtaja Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani na kusema kuwa wamekua wakitoa majibu ya uongo bungeni na ambayo hawayafanyii kazi.

"Mhe Spika Mawaziri wetu wamekuwa wakitoa majibu mazuri ambayo yanaturidhisha sisi wabunge, kwa mfano majibu ya mjomba wangu Mwijage anatoa majibu kana kwamba Mungu yupo hapa lakini wakitoka hapa yale majibu hawatekelezi huko, lakini ukimbana sana atakwambia kuwa akitoka bungeni ataongozana na wewe mpaka jimboni kwako lakini mkishamaliza bunge hata simu hapokei na hilo suala la kuja jimboni halipo" alisema Mlinga.

Mbunge huyo aliendelea kutaja Mawaziri ambao ni waongo "Mhe mwingine ni Kalemani naye anakwambia baada ya bunge atakuja jimboni kwako ili kukuridhisha wewe Spika na kuniridhisha mimi mbunge, Mh Spika naomba bunge lituelekeze namna nyingine ya kuweza kuwabana hawa watu ili waweze kuwajibika kutokana na wajibu yao ya uongo" alisisitiza Mlinga.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata