UKATILI WA KUTISHA:MWANAMKE AUWAWA NA MWILI WAKE KUTELEKEZWA KWENYE PAGALA.

Mwanamke mmoja amekutwa akiwa ameuawa na watu wasiyofahamika na mwili wake kutupwa kwenye nyumba ambayo haijamalizika kujengwa (Pagala) huku akiwa amefungwa kwenye mfuko wa sandarusi na kuzungushiwa nguo alizokuwa amevaa.

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoani Mwanza, DCP Ahmed Msangi na kusema tukio hilo limetokea tarehe 16.08.2017 majira ya saa 11:30 jioni katika mtaa wa Kitangiri kata ya Kitangiri Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

DCP Msangi amesema mwili wa marehemu uliweza kuonekana mahali hapo baada ya watoto waliokuwa wakicheza eneo hilo kuona kifurushi kilichotupwa kwenye Pagala ndipo walipotoa taarifa kwa mama yao na baadaye kutoa taarifa kwa uongozi wa Mtaa pamoja na kituo cha Polisi.

Aidha, Kamanda Msangi amesema mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote bali uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa wauaji walimuua kwa kumziba pumzi kisha kwenda kumtupa kwenye Pagala eneo ambalo siyo rahisi mtu kupita.

Kwa upande mwingine, DCP Msangi amesema upelelezi unaendelea wa kuwatafuta watu waliyohusika na mauaji ya mwanamke huyo kwa namna moja ama nyingine. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata