MWANASHERIA MKUU AIOMBA MAHAKAMA IMUUNGANISHE KWENYE KESI YA FIDIA YA MH MBOWE.


AG,GEORGE MASAJU.
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG) ameiomba Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, kumuunganisha katika kesi ya madai ya fidia ya zaidi ya Sh. nusu bilioni iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe dhidi ya Gelasius Byakanwa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Hai.

Kesi hiyo ya ardhi namba 20 ya mwaka 2017, ilifunguliwa na Kampuni ya Kilimanjaro Veggie Limited (KVL) inayomilikiwa na Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai dhidi ya Byakanwa kama mtu binafsi na si kwa cheo chake.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Bernard Mpepo aliiambia Nipashe jana kuwa ombi hilo la AG, ambaye kwa sasa ni George Masaju, itabidi lisubiri, hata hivyo, mpaka tarehe nyingine ya kesi hiyo.

“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali walifika leo (jana) mahakamani wakiomba kuunganishwa lakini haikuwezekana," alisema Mpepo.

"Kwa hiyo ombi lao watalitoa rasmi mahakamani Septemba 5, mwaka huu wakati kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa rasmi saa 3:00 asubuhi.”

Kesi hiyo ambayo imekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii haikusikilizwa jana kama ilivyokuwa imepangwa awali kutokana na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aishiel Sumari kuiahirisha ili aendelee na kesi za dawa za kulevya.

KVL inadai kuwa Juni 19, mwaka huu Byakanwa aliharibu miundombinu ya umwagiliaji wa shamba kitalu (green house) lake. Mbowe ndiye Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni hiyo.

Ni mara ya pili kwa AG kuomba kuunganishwa katika kesi hiyo baada ya Julai 13 wakili wa Byakanwa, Modestus Njau kutaka iwe hivoy.

Katika kesi hiyo, Mbowe anawakilishwa na wakili Meirad D’souza.

Katika hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili D’Souza, Mbowe analalamikia kitendo cha Byakanwa kuingia kwa jinai katika shamba hilo na kufanya uharibifu.

Mbowe anadai kuwa Byakanwa hakuwa na mamlaka ya kisheria kufanya alichokifanya na kuiomba mahakama itoe zuio la kudumu kwa Byakanwa kutoingilia shughuli za KVL.

Mbowe anaiomba Mahakama imuamuru Byakanwa kumlipa fidia ya Sh. milioni 549.3 inayotokana na uharibifu wa mali, usumbufu na hasara ambayo KVL imepata.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata