MBIVU NA MBICHI ZA RAILA KUJULIKANA

Kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, leo anatarajiwa kuwaeleza wafuasi wake mwelekeo atakaochukua baada ya kutangaza kuwa hatambui ushindi wa rais Uhuru Kenyatta, baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wiki iliyopita.

Bw.Odinga ambaye amewania urais mara nne, amekuwa akishauriwa kwenda Mahakamani, kushtaki madai yake, lakini muungano wake wa upinzani National Super Alliance (NASA) , umesema hautakwenda Mahakamani.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Bw. Odinga  alitoa wito kwa wafuasi wake kutokwenda kazini  siku ya Jumatatu ambapo agizo hilo lilikaidiwa kwa watu kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Hata hivyo Shughuli za kawaida zimeanza kurejea polepole katika miji mbalimbali nchini humo.

Pamoja na hayo jana Rais mteule wa Kenya Mh Uhuru Kenyatta alitoa ruhusa kwa watu wanaopinga ushindi wake kuandamana  huku akitoa angalizo kwa watakaoharibu mali za umma kuwa hawatavumiliwa.

Vilevile Sherehe za kumuapisha Uhuru Kenyatta zinategemea kufanyika Agosti 29 ikiwa ni ndani ya siku 14  baada ya mshindi wa uchaguzi kutangazwa ili kutoa fursa kwa chama chochote kinachotaka kupinga matokeo kufanya hivyo kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata