MAHAKAMA YAIJIA JUU TANROADS KWA KUBOMOA NYUMBA ILIYOZIPA KINGA

Baada ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kubomoa baadhi ya nyumba zilizowekewa kinga ya muda, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imesema hilo ni kosa la kuupuza amri ya mahakamana na kueleza hatua ambazo waathirika wanapaswa kuzichukua.

Msajili wa mahakama hiyo, Frank Mahimbali jana alisema kuwa wanachoweza kufanya waathirika ni kwenda mahakamani kuomba iwaite waliohusika na ubomoaji huo ili wajieleze ni kwa nini wasifungwe kwa kupuuza amri ya mahakama.

Mahimbali alisema mtuhumiwa akitiwa hatiani anaweza kufungwa jela.

Ijumaa iliyopita, mahakama hiyo ilitoa amri ya zuio la muda la ubomoaji kwa nyumba 286 zilizoko katika operesheni ya bomoabomoa maeneo mbalimbali kati ya Ubungo Maji na Kiluvya, zilizojengwa ndani ya umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya Barabara ya Morogoro.

Amri hiyo ilitolewa na Jaji Leila Mgonya baada ya maombi ya dharura yaliyowasilishwa na wakazi 286 wa maeneo hayo, wakiomba mahakama itoe zuio nyumba zao zisibomolewa kusubiri kesi yao ya msingi itakapoamuriwa.

Hata hivyo, juzi Tanroads ilibomoa nyumba tatu katika eneo la Kimara Stop Over, ambazo ni kati ya hizo 286. Nyumba hizo zilizobomolewa ni pamoja na Nicomed Leo na ya Aisha Juma.

Wakati mahakama ikitoa msimamo na maelekezo hayo kwa waathirika wa bomoabomoa hiyo ambao nyumba zao zimewekewa kinga hiyo, wakili wao Benedicto Mandele alisema jana kuwa tayari wameshamwandikia barua Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kueleza malalamiko yao na hatua wanazopanga kuzichukua.

Wakili Mandele alisema katika barua hiyo ambayo pia nakala yake imetumwa kwa Jaji Mgonya, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Saalam, Ofisa Mtendaji wa Tanroads, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kinondoni, wateja wake wameeleza kusikitishwa kwao na kitendo hicho wakati kuna amri ambayo ilibandikwa kwenye nyumba hizo.

“Tayari barua hiyo imepokewa leo (jana) saa nne na sasa hapa ninaandaa maombi kwa ajili ya kumuita meneja wa mkoa wa Tanroads afike mahakamani kujieleza ni kwa nini asifungwe jela kama mfungwa wa kesi ya madai kwa kupuuza amri ya mahakama,” alisema Wakili Mandele na kuongeza kuwa maombi hayo dhidi ya meneja huyo wa Tanroads atapeleka mahakamani leo baada ya wateja wake kuweka saini.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata