BILL GATES AANZA KUINADI TANZANIA

SIKU chache baada ya taasisi ya Bill na Bellinda Gates kuitengea Tanzania Dola za Marekani milioni 350 (takribani Sh bilioni 777), Mwenyekiti mwenza wa taasisi hiyo ambaye ni tajiri namba moja duniani, Bill Gates amezidi kuipaisha Tanzania kwa kuinadi kimataifa.

Fedha zilizotengwa na taasisi hiyo ni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo ya kilimo, afya na mifumo ya elektroniki ya upatikanaji wa taarifa, Safari hii, Gates ambaye jina lake halisi ni William Henry Gates III, kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram alioufungua akiwa nchini kwa jina la thisisbillgates, ameinadi Tanzania akielezea jinsi anavyoguswa na nchi inavyopiga hatua kwa kasi katika kuendeleza sekta ya afya na kutoa fursa katika maeneo mbalimbali, huku akirusha picha tatu za kwanza alizopiga akiwa Kicheba, wilayani Muheza, mkoani Tanga.

Jarida maarufu la uchumi la duniani, Forbes Marekani ndilo lililoripoti juu ya Gates kujiunga na mtandao wa Instagram akiwa nchini na kuelezea anavyoguswa na ustawi wa Tanzania kwa ujumla.

Hayo yameripotiwa kupitia katika ujumbe wake huo ulioandikwa kwa lugha ya Kiingereza, sehemu ya ujumbe wake ameweka maneno yanayotafsiriwa; “Hello kutoka Tanzania, Instagram! Nimepata chakula kizuri cha mchana nikiwa na watoto wanaovutia katika Shule ya Msingi Kicheba, Muheza na nikakutana na Upendo Mwingira ambaye amejikita katika kupambana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele.

“Mimi na Melinda tumekuwa tukija Tanzania kwa miaka mingi sasa. Huwa napenda kuona maendeleo ambayo nchi imeyafanya katika kuboresha afya na kutoa nafasi.” Kauli ya Gates, mwanzilishi, mwenyekiti na mbunifu mkuu wa programu za kampuni ya Microsoft, kampuni ya programu yenye mafanikio zaidi duniani inayoaminika kwa utengenezaji wa programu zilizo na nguvu na ubunifu wa hali ya huu, mapema wiki hii, alielezea kufurahishwa na maendeleo ya uchumi wa Tanzania pamoja na uongozi na msimamo wa Rais John Magufuli juu ya kutaka miradi ya maendeleo iwe na tija kwa jamii.

Aliyasema hayo alipokutana na Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam mapema wiki hii na kuongeza kuwa, kutokana na imani aliyonayo kwa Tanzania, atakuja nchini mara nyingi ili kuimarisha zaidi ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi.

Naye Rais Magufuli, akimshukuru Gates kwa imani aliyonayo kwa Tanzania na pia kwa fedha alizotoa ili kutekeleza miradi mbalimbali nchini, alisema; “Tunamshukuru sana (Bill Gates), ameamua mwenyewe kutuletea hizi fedha na anasema tunaenda vizuri.

Kwa hiyo ameona hana mahala pa kuzipeleka hizi hela anazileta Tanzania kwa sababu tunajua kuzitumia. “Hataki hela yake anaihangaikia kule halafu inakuja hapa inatumika ovyo. Tumemueleza hatua zetu na amekuwa akizisikia, anaziona hatua tunazochukua za kupambana na Ufisadi.”

Bill Gates mwenye umri wa miaka 61 sasa, alipata utajiri katika na umri mdogo kiasi cha kumfanya kuwa bilionea akiwa na miaka 31 tu. Ana utajiri wa Dola za Marekani bilioni 86 (Sh trilioni 180).

Pamoja na utajiri wake, bilionea huyo asiye na makuu, amekuwa akisisitiza kipato alichojaliwa na Mungu atakitumia kwa faida ya watu wengi zaidi kupitia miradi mbalimbali ya kijamii duniani, huku akisisitiza fedha zake hazitarithiwa na watoto wake watatu, Jennifer Katharine (21), Rory John (18) na Phoebe Adele (15).

Kuhusiana na watoto wake, aliwahi kusema: “Watoto wetu watapata elimu nzuri na kiasi cha fedha ili wajue pa kuanzia wasije kufa masikini. Si tabia njema kuwarithisha watoto mali, bali kuwapa njia ya kutafuta mafanikio yao kwa nguvu na akili zao”.

Anaishi katika kijiji chake huko Medina, Washington alichokijenga kwa miaka 7 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 63 (Sh bilioni 132.3), na kwa sasa kina thamani ya Dola milioni 125 (Sh bilioni 262.5).

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata