ANUSURIKA KIFO BAADA YA KUPAMBANA NA CHUI KAVU KAVU.Na. Ahmad Mmow, Lindi.

MTU mmoja mkazi wa kijiji cha Maziwa,wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, anaetambulika kwa jina la Hamidu Hussein (51), amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na chui shambani kwake.

Akieleza tukio hilo mmoja wa ndugu zake ambae hakutaka jina lake liandikwe, kwamadai kuwa sio msemaji wa serikali wala ukoo, alisema Hamidu ambae ni mkazi wa kijiji Maziwa alivamiwa na chui huyo baada ya kukutana nae uso kwa uso akiwa kwenye shamba lake la mikorosho lililopo katika kijiji cha Mbondo tarafa ya Kilimarondo.

" Ingawa alikuwa na panga lakini lilimdondoka kabla ya kukabiliana na chui huyo kwa kutumia mikono bila kifaa chochote, waliburuzana kipindi kirefu sana. Hata hivyo mtu mmoja baada ya kusikia sauti ya kuomba msaada alikwenda na kumsaidia nakufanikiwa kumuuwa chui yule, "alisema.

Ndugu huyo aliongeza kusema tukio hilo lililosababisha watu wengi kufurika zilipo ofisi za idara ya maliasili ya halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, ili kumuona chui huyo, alisema lilitokea majira ya saa kumi alasiri jana.

" Alimshika shingoni baada ya kufanikiwa kumtatua toka miongoni, alipofika huyo mtu ilikuwa nirahisi kumpiga kwa upanga ule, kwasababu Hamidu alishamdhibiti kisawasawa, "alisisitiza.

Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Nachingwea, Dk Ibrahim Pazia, alikiri kuwa Hamidu alipelekwa katika hosipitali hiyo na anaendelea kutibiwa majeraha yaliyotokana na mnyukano huo.

Dk Pazia ambae pia ni mganga mfawidhi wa hosipitali hiyo alisema ,Hamidu aliumizwa sana maeneo ya usoni na kuvuja damu nyingi. Hali iliyosababisha aongezwe damu uniti  (chupa) moja na kushonwa nyuzi kadhaa.

"Aliletwa akiwa huwezi kusema, ila sasa anaweza kusema na anaendelea vizuri, "alisema Dk Pazia.

Nae mkuu wa idara ya maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Lington Nzunda, alithibitisha kuwa ni kweli chui huyo aliuwawa na kupelekwa katika ofisi ya idara hiyo. Ambapo kazi ya za kumchuna ngozi ilikuwa inaendelea.

" Aliletwa hapa, akishachunwa ndipo mwili wake tutauchoma moto. Sisi tunachohitaji ni ngozi tu, "alisema Nzunda.

Juhudi za kuwapata viongozi wa kijiji na kata ya Mbona, ili wathibitishe kutokea tukio hilo kwenye maeneo ya utawala ziligonga mwamba, baada ya kushindwa kupatikana kila walipopigiwa simu. 

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata