WANANCHI WARUHUSIWA KUENDELEA NA SHUGHULI ZA UVUVI KWENYE BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU

Wakuu wa mikoa  ya Kilimanjaro na Manayara wamefungua bwawa la nyumba ya Mungu na kuruhusu shughuli za uvuvi ambazo zilikuwa zimezuiliwa kwa muda wa mwaka mmoja kutokana na kushamiri kwa uvuvi haramu ambao ulihatarisha uwepo wa samaki katika bwawa hilo.

Akizungumza na wananchi waozunguka bwawa la nyumba ya Mungu katika kijiji cha Spillway katika wilaya ya Mwanga mkuu wa mkoa wa Manyara Bw. Joel Bendera amesema shughuli za uvuvi katika bwawa hilo zitafanyika kwa kipindi cha miezi sita .

Amesema pamoja na kuruhusu shughuli za uvuvi katika bwawa hilo kwa wavuvi watakaobainika kuvua samaki kwa kutumia vyandarua watachukuliwa hatua za kisheria ili kuwezesha samaki kuendelea kuzaliana na kukua.

Katika zoezi hilo pia  nyavu zaidi ya 300 ziliteketezwa ambapo mkuu  mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mghira amewataka wavuvi kufuata sheria na kutumia nyavu zilizoanishwa kisheria kwa ajili ya uvuvi na  kwamba kwa wananchi waliojenga ndani ya mita siti kutoka kwenye bwawa hilo wataondolewa.

Nao baadhi ya viongozi wa vijiji na wananchi wanaotegemea shughuli za uvuvi katika bwawa la nyumba ya Mungu wamepongeza hatua ya kufunguliwa kwa bwawa hilo na kuiomba serikali kuangali uwezekano wa kuwapelekea nyavu kubwa ambazo zinafaa kwa uvuvi ili kuepuka kutumia vyandarua.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata