WAHENGA WA ESCROW WAZIDI KUIBUKA

ALIYEKUWA MWENYEKITI WA PAC ZITTO KABWE AKIWA NA DEO FILIKUNJOMBE WAKIMKABIDHI JOB NDUGAI RIPOTI YA TEGETA ESCROW.

SIKU moja baada ya Tundu Lissu na David Kafulila kutaka watu wote waliopata mgawo wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow miaka mitatu iliyopita wakamatwe na kushtakiwa mahakamani.

'mhenga' mwingine aliyekuwa mstari wa mbele kufichua kashfa hiyo, Zitto Kabwe, amefunguka na kusema mazito kuhusu sakata hilo.

Baada ya William Ngeleja kutangaza Jumatatu kurejesha kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) mgawo wake wa Sh. milioni 40.4 zinazodaiwa kuwa zao la kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya akaunti ya Tegeta Escrow, Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Lissu alisema juzi kuwa Mbunge wa Sengerema (CCM) huyo na watu wote waliopata mgawo huo wanatakiwa kukamatwa na kushtakiwa kwa kuwa ameuthibitishia umma kuwa ni mla rushwa.

Kauli hiyo ya Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliungwa mkono na Kafulila ambaye ndiye aliyeibua kashfa hiyo bungeni, kipindi hicho akiwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi).

Alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia suala hilo, Zitto alisema sakata la akaunti ya Tegeta Escrow ni kubwa zaidi ya kurejeshwa kwa fedha hizo.

Zitto (40), ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama hicho, aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhakikisha inafuatilia kila senti iliyotoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na ilikopelekwa.

Alisema wahusika wote, walioiba na waliowasaidia wezi ni lazima wakamatwe, huku akieleza kuwa mitambo ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) bado iko chini ya kampuni hiyo licha ya Bunge kuazimia itaifishwe.

Kutokana na mazingira hayo ya mitambo kuwa bado chini ya IPTL, nchi bado inalipa mabilioni ya Shilingi kwa kampuni hiyo, alisema zaidi.

"Kashfa ya Escrow ni kubwa kuliko kitendo cha kurejesha pato la uhalifu. Takukuru ni lazima ifuatilie kila senti iliyoibwa kutoka Tegeta Escrow mpaka ilipoishia," alisema na kueleza zaidi: "Baada ya hapo, washtakiwe wote, wale walioiba na wale waliosaidia wezi.

Mitambo bado ipo mikononi mwa IPTL, bado tunalipa mabilioni ya shilingi kama tozo ya uwekezaji. Hilo ndilo jambo kubwa tunalopaswa kulizungumzia." Mbali na Zitto, Kafulila na Lissu, wabunge wengine waliokuwa mstari wa mbele kulisimamia sakata hilo bungeni mwaka 2014 ni marehemu Deo Filikunjombe, aliyekuwa Mbunge wa Ludewa (CCM) na Kangi Lugola, Mbunge wa Mwibara (CCM).

Katika ripoti yake iliyowasilishwa kwenye Kikao cha 18 cha Bunge la 10, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilianika majina ya maofisa wa serikali, wabunge na viongozi wa dini waliopata mgawo wa fedha.

Watu hao walipewa fedha hizo na Mkurugenzi wa VIP Engineering na mmiliki mwenza kwa kampuni ya IPTL, James Rugemalira.

Mkurugenzi huyo na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Power African Power (T) Limited (PAP), Habinder Sethi Sigh wako mahabusu kwenye Gereza la Keko jijini baada ya kukosa dhamana walipofikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wiki iliyopita na kusomewa mashtaka 12, yakiwamo ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309.4.

Mbali na Ngeleja, watu wengine waliopata mgawo huo ni ofisa katika Ofisi ya Rais wakati huo, Shabani Ngurumo aliyepewa Sh. milioni 80, aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Eudes Ruhangisa Sh. milioni 404.25 na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), Dk. Enos Bukuku Sh. milioni 161.7.

Katika ripoti hiyo Waziri wa Nishati na Madini wa serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, Mbunge wa zamani wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Aloisius Mujulizi walitajwa kupatiwa Sh. milioni 40.4 kila mmoja.

Wengine ni Ofisa wa TRA, Lucy Apollo Sh. milioni 80.8, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko milioni 40.2, maaskofu Methodius Kilaini Sh. milioni 80.9 na Eusebius Nzingirwa 40.4, Padri Alphonce Twimannye Sh. milioni 40.4, maofisa wa Rita Placidus Luoga Sh. milioni 121.2 na Theophil Rugozobwa Sh. milioni 323.4.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata