MBUNGE WA USHETU MH KWANDIKWA ATOA MIKAKATI YA KUPAMBANA NA FISI WANAOHATARISHA MAISHA YA WANAFUNZI JIMBONI KWAKE.Halmashauri ya ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga imekuja na na mikakati ya kupambana na fisi wanaohatarisha maisha ya wanafunzi wanaosomea umbali mrefu kwa kujenga shule na kumalizia maboma ya shule yaliyotelekezwa.

Akiongea na Kijukuu Blog mkoani Dodoma,Mbunge wa jimbo la Ushetu Elius Kwandikwa amesema kuwa wamejipanga kumaliza tatizo hilo kwa kusogeza shule karibu na jamii ambazo zilikuwa zikipata huduma hiyo katika umbali mrefu.

Kwandikwa amesema kwa sasa shule saba zipo kwenye umaliziaji katika kata sita za jimbo hilo huku mkazo ukiwekwa katika vijiji ambavyo havikuwa kuwa na shule kabisa.

“Tumeaanza ujenzi na maendeleo ni mazuri katika kata sita na tunaamini shule zitakamilika kwa wakati katika maeneo yote ambayo ujenzi huo unafanyika” Alisema Kwandikwa.

Akizitaja shule ambazo zinajengwa na kukarabatiwa Kwandikwa amesema kuwa ni pamoja na Ntungulu iliyopo kata ya Chambo,Mikwa iliyopo kata ya Mapamba,Mliza katika kata ya Bukomela pamoja na Nondwe iliyopo eneo la Bukale kata ya Bulungwa.

Shule zingine zilizo katika mpango huo Kwandikwa amezitaja kuwa ni Nyabusalu iliyopo kata ya Bulungwa,Shule ya Nabe Iliyopo katika kata ya Ubangwe pamoja na shule ya Bugela iliyopo kata ya Ulowa.

Akizungumzia umbali unavyoathiri maendeleo ya Elimu Ushetu,Mh Kwandikwa amesema kuwa watoto wengi hawaudhurii masomo kutokana na umbali na woga wa kuvamiwa na wanayama wakali.

“Watoto hawaendi shule kutokana na umbali lakini pia wazazi wanawazuia wasiende shule wakihofia watoto wao kuvamiwa na wanyama wakali,sasa hali hii kwa kweli inasabisha kushuka kwa maendeleo ya wanafunzi” Alisema Mbunge Kwandikwa.

FISI WANAODAIWA KUHATARISHA MAISHA YA WANAFUNZI JIMBO LA USHETU.

Kuhusu changamoto zingine zinazokwamisha maendeleo ya shule kwa jimbo la Ushetu,Mh Kwandikwa amesema kuwa ni pamoja na utoro,Kuhama hama kwa wazazi kwa ajili ya kilimo na Ufugaji,Baadhi ya wazazi kuwahamisha watoto wao kufuata fursa za shule nzuri za mjini pamoja na Mimba kwa wanafunzi wa kike.

Sambamba hayo Mh Kwandikwa amesema kuwa katika kuhakikisha wanatokomeza mimba kwa wanafunzi wanajipanga kujenga mabweni ambayo wanafunzi wa kike watakuwa wanaishi na kusimamiwa na uangalizi.

Katika kuboresha miundo mbinu ya Shule Mh Kwandikwa amesema kuwa wanajipanga kuvuta umeme katika shule nyingi za sekondari kupitia mradi wa umeme vijijini Rea.

Kuhusu utayari wa wazazi na jamii katika kuchangia miradi ya maendeleo Kwandikwa amesema kuwa wazazi wako tayari na wanapenda watoto wao wapate elimu.

“Utayari wa wazazi ni mkubwa na wanapokea mawazo na wanashirikiana vyema na serikali katika kujenga madarasa na nyumba za walimu,na wanapenda watoto wao wasome ni wazazi wachache sana ambao hawatoi ushirikiano”Alisema Kwandikwa.

Kuhusu uchache wa walimu wa masomo ya Sayansi Mbunge Kwandikwa amesema amejipanga kuwakusanya wanachuo wanaosomea masomo ya Sayansi wanaotokea Ushetu kurudi kufundisha katika shule zenye uhaba wa walimu hao kwa kuwalipa ujira kidogo wakati wanapokuwa katika vipindi vya mapumziko.

 Akizungumzia mipango ya mbeleni katika kukuza Elimu Ushetu,Mh Kwandikwa amesema kuwa wana mipango ya kuwa na Chuo cha Ufundi ambapo kwa sasa wanafanya mazungumzo na wizara ya elimu ili kuweka mikakati ya kuanza ujenzi wa chuo hicho.

Swala  la walimu kujiingiza katika kilimo cha Tumbaku na Mpunga hali inayowafanya washindwe kutimiza majukumu yao ya kufundisha na kusalia kwenye kilimo Mh Kwandikwa amesema kuwa wao waendelee na kilimo ila kilimo chao kisiingiliane na muda wa kazi.

“Unajua Ushetu ni kijijini na tuna udongo wenye rutuba nzuri sana,hivyo mtu hawezi kuishi ushetu akashindwa kufanya shughuli za kilimo,Walimu na wafanyakazi wengine wa halmashauri ruksa kufanya shughuli za kilimo lakini wasichanganganye muda wa kazi na shughuli binafsi” Alisema Kwandikwa.

Kwa upande wao baadhiya wazazi wameiambia Kijukuu Blog kuwa kwasasa wanapata faraja kubwa kwa uanzishwaji wa shule hizo kwani walikuwa na hofu kubwa kwa watoto wao kwenda umbali mrefu kusoma.

Wameongeza kuwa inafikia wakati wanaacha kufanya shughuli za maendeleo na badala yake wanalazimika kuwasindikiza watoto wao shuleni na kisha kuwafuata jioni ili wasipate madhara njiani.

Siku za hivi karibuni kumeripotiwa kuwa na fisi wanaohatarisha maisha ya watu katika halmshauri za Msalala na Ushetu hali ambayo inatajwa kuhatarisha maisha ya watu hususan wanafunzi wanaosafiri umbali mrefu kufuata Elimu.SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata