MAKONTENA 10 YA KEMIKALI BASHIRIFU ( ETHANOL )YAKAMATWA BANDARINI

Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini imekamata makontena 10 yaliyokuwa na kemikali aina ya ethanol yenye ujazo wa lita 200000 (Laki mbili) kupitia bandari ya Dar es salaam kutokea nchini Swaziland.

Taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa kupambana na dawa za kulevya nchini Rogers Sianga inasema kuwa kemikali ziliingizwa nchini na kampuni ya 'Hamid Ibrahim Saambaya' na kusema kwamba makontena hayo yamekamatwa kutokana na kampuni hiyo kutofuata miongozo na ya sheria zilizopo kutoka katika mamlaka husika za kujihusisha na kemikali bashirifu.

Taarifa ya Sianga imedai kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiingiza kemikali hizo nchini tangu mwaka 2016 na kufikia jumla ya ujazo wa lita milioni moja na nusu na kwamba kampuni hiyo haijawahi kusajiliwa wala kuweka kumbukumbu wapi kemikali hizo zinakopelekwa.

"Pamoja na kwamba kemikali hizo zinatumika kwa matumizi mengine viwandani kama kutengeneza pombe na vinginevyo pia kwa kutumia kemikali hizi zikichepushwa zinaweza kutengeneza dawa za kulevya" Taarifa iliyotolewa na Kamishna Sianga ilieleza.

Hata hivyo mamlaka kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinaendelea na uchunguzi juu ya uhalali wa biashara za kampuni hiyo na kufahamu mahali sahihi kemikali hizo zinapopelekwa na baada ya hapo hatua za kisheria zitachukuliwa.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata