MAAJABU:KITANDA CHA RAIS MAGUFULI CHAPOTEA.

Moja kati ya vitanda vitano ambavyo Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli alivitoa kwa halmashauri ya wilaya ya Mkalama mkoani Singida kwa ajili ya kujifungulia akina mama wajawazito kimepotea katika mazingira ya kutatanisha.
 
Upotevu huo umetajwa kwenye risala fupi kwa mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Mkalama Eng. Jackson Masaka, kwenye hafla ya makabidhiano ya vitanda vinne (4) vya kujifungulia, vitanda 20 vya kupumzikia wagonjwa, magodoro 20  na mashuka 50. Vitanda vya kujifungulia vilipaswa kuwa vitano(5).
 
Vitanda hivyo na mashuka hayo, ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk. Magufuli, kwamba katika kipindi chake cha uongozi hakutakuwa na mgonjwa yeyote katika nchi hii, atakaye lazwa sakafuni kwa kukosa kitanda na godoro, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
 
Akizungumza kwenye hafla hiyo fupi ya makabidhiano hayo, DC Eng. Jackson Masaka, aliangiza juhudi zifanyike mapema iwezekanavyo, ili kitanda hicho kipatikane na apewe taarifa ya kufanikisha agizo hilo.
 
Aidha, alisema serikali ya awamu ya tano imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za afya nchini, ili wananchi wapate huduma bora za afya, waweze kushriki kikamilifu katika shughuli zao za kujiletea maendeleo.
 
“Binafsi na kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Mkalama, tunamshukuru rais wetu Magufuli kwa juhudi kubwa anazofanya katika kuimarisha huduma za afya nchini. Tunaomba Mungu amjalie afya njema, ili aendelee kuongoza na kuwaletea maisha bora Watanzania,” alisema Eng. Masaka.
 
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya, amewataka wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF), ili kujijengea mazingira mazuri ya kupata matibabu hata kipindi hawana fedha.
 
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Mkalama, Allan Kiula, pamoja na kushukuru kwa msaada huo wa vitanda na mashuka, ametumia fursa hiyo kuiomba serikali isaidie ujenzi wa hospitali ya wilaya ili kupunguza adha kwa wagonjwa wanaopata rufaa ngazi ya wilaya kufuata huduma, nje ya wilaya.
 
Awali Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mkalama, Dk. Deogratias Masini katika risala yake alitaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni ukosefu wa ‘ambulance’ kwa ajili ya wajawazito.
 
Alitaja zingine kuwa ni wilaya kutokuwa na hospitali,kukosa kituo cha afya cha kutoa huduma za upasuaji, akina mama wajawazito kujifungulia nyumbani, uhaba wa watumishi wa afya na ushiriki mdogo wa wanaume kuhudhuria kliniki na wenza wao.
 
Hata hivyo, Dk. Masini ambaye ni mganga mkuu wa wilaya ya Mkalama,alisema pamoja na changamoto hizo, yapo mafanikio waliyopata katika kipindi cha mwaka jana,ambapo hakuna vifo vya akina mama wajawazito na pia lipo ungezeko kubwa la akina mama wajawazito, kujifungulia kwenye vituo vya afya.
 
Mkazi wa Nduguti wilaya ya Mkalama, Habiba Issa, ameiomba  serikali ifanye juhudi ya kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya, vinakuwa na wahudumu wa kutosha.
 
Serikali kupitia wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto imeagiza bohari ya dawa (MDS) kusambaza vitanda vya hospitali 20, magodoro 20, vitanda vitano vya kujifungulia akina mama wajawazito na mashuka 50, katika kila Halmashauri ya wilaya Nchini.
 
Thamani ya vitanda, magodoro na mashuka hayo, ni zawadi ya shilingi 2.9 bilioni.
Na Nathaniel Limu, Mkalama

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata