KONTENA HEWA LAMTIA MATATANI

KONTENA hewa la simu za IPhone 7 limemfi kisha mahakamani Mkurugenzi wa Kampuni ya Candy & Candy, Josiah Kairuki (38) mkazi wa Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Kairuki ambaye ni raia wa Kenya, anatuhumiwa kujipatia Sh milioni 336 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Yusuph Mohamed ili akomboe kontena hilo katika Bandari ya Dar es Salaam, kitu ambacho ni uongo.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Anzelini Muhela, alieleza mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Longido, Aziza Temu kuwa mtuhumiwa huyo amejipatia fedha hizo kati ya Januari 23 na Juni 10, 2017.

Mwendesha Mashitaka alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na aliomba mtuhumiwa huyo asipewe dhamana kwani uraia wake una utata, hivyo akiwa nje anaweza kusababisha kupotea kwa nyaraka za kesi, kutoweka na kiasi alichojipatia ni kikubwa.

Hata hivyo, Wakili wa Kairuki, John Mallya alipinga hoja zote za mwendesha mashitaka na kueleza dhamana ni haki ya kikatiba ya mtuhumiwa ambaye hajatiwa hatiani. Hakimu Temu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 26, mwaka huu ambapo atatoa maamuzi ya kumpa dhamana mtuhumiwa huyo ama kutompa.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata