WANANCHI WASUSIA UTAFITI WA MADINI MASASI


Wananchii wa Kijiji cha Chiwata kilichopo Ndanda Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wamekataa mchakato wa utafiti wa uchimbaji  madini kutokana na kile walichokidai ni  kutoshirikishwa katika ufanyaji wa tathmini ya mashamba yao.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara ilioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Ndanda, Cecil Mwambe, baadhi ya wananchii wa kijiji hicho wamesema kampuni ya utafiti ya NACHI Resources ilianza kazi bila kuwashirika hivyo kuomba mchakato huo kusitishwa mpaka pale watakaposhirikishwa.

Wamedai kuwa tathmini inaelekeza malipo ya Sh 200,000 hadi Sh 400,000  kwa heka moja jambo ambalo wanalipinga ingawa bado uchimbaji wa madini haujaanza.

Mmoja wa wananchi hao, Habiba Hashim, akizungumza katika mkutano huo huku akiwa amepiga magoti, alisema baada ya mchakato huo kuanza waliitisha mkutano wa kijiji na kukataa uwekezaji huo hadi watakaposhirikishwa.

"Tulikaa kwenye mkutano wa kijiji tukakataa, kwa kifupi mbunge napiga magoti kwa mara ya pili, sikiliza kilio cha wanaChiwata, mgodi hawautaki chonde wasikilize mama zako, bibi zako na kaka zako, "alisema Hashim

Kwa upande wake Ismail Liganga mkazi wa Chiwata alisema hawana ugomvi na kampuni hiyo isipokuwa wanataka haki itendeke.

"Kampuni ya Nachi Resources tunawaomba sisi sio wagomvi wenu isipokuwa tunataka mtambue kwamba sisi tulikuwa tunalima kwenye ile ardhi tunapata thamani kubwa na maendeleo, tunasomesha watoto wetu leo mnachukua kwa laki mbili sisi tukaishi wapi?” Alihoji Liganga.

Mwakilishi wa Kampuni ya Nachi Resources, Peter Dodi  alisema taratibu zote zilifuatwa kuanzia utafiti na hakuna walipokiuka sheria za nchi na tofauti zilizopo ni pale watu wanapokosa taarifa sahihi, huku Mwambe akisema wananchi hao hawana uwezo wa kuzuia kuanza uchimbaji isipokuwa inatakiwa yawepo maridhiano baina ya serikali, wawekezaji na wananchi.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata