WAISHI MLIMANI KUKWEPA OPERESHENI YA KUSAKA WALIMA MIRUNGI

Mamia ya wananchi wanaodaiwa kujishughulisha na kilimo cha mirungi katika vijiji vitatu vya wilayani Same, wamekimbia makazi yao na sasa wanaishi porini kukwepa operesheni ya kusaka wakulima wa miche hiyo ya kulevya.

Wananchi hao wamekimbilia maeneo ya milimani na kutelekeza watoto ambao sasa wanalala nje. Jitihada za vyombo vya usalama kuwafikia zimeshindikana kutokana na urefu wa milima.

Eneo hilo la ukanda wa milimani katika wilaya hiyo ya Same, lina mazingira ya baridi kali katika kipindi hiki, hali ambayo inawafanya watoto na wanafamilia wanaolala nje kuwa hatarini kuathirika.

Wakati wananchi hao wakizikimbia nyumba zao, Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya imetangaza kupanua operesheni katika mikoa minne.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamle aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa vijiji ambavyo wananchi wake wamekimbilia porini ni Tahe, Ekonte na Rikweni.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, operesheni hiyo ilianza usiku wa Juni 14 na kukamilika Juni 16 na kwamba hadi wanamaliza wakimbizi hao walikuwa hawajarejea kwenye makazi yao.

“Katika vijiji hivyo wahalifu walikimbilia milimani, hali iliyovifanya vyombo vya ulinzi na usalama kushindwa kuwakamata kirahisi kutokana na jiografia ya wilaya ilivyo,” alisema.

“Wote watatafutwa na kushughulikiwa. Wang’oe mirungi kwa hiyari yao. Viongozi wa vijiji na kata waendelee kuwashika wale ambao hawajang’oa mirungi.

“Tanzania ni ya amani lakini wameamua kujipotezea amani kwa kulala porini. Ni kama vile wako vitani. Wale wote wanaowatesa watoto kwa kuwalaza nje, tutawasaka na kuwakamata”.

Katika operesheni hiyo, vyombo vya ulinzi na usalama vilifanikiwa kukamata wakulima sita wa kilimo hicho, baada ya mamia kupeana taarifa kwa simu wakati vikosi vikianza kupanda mlima.

Pia vikosi vilivyokuwa vikishiriki operesheni hiyo, viliteketeza ekari 48 za mashamba ya kilimo cha mirungi. Kulima mirungi ni kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah aliwataka wananchi wote wanaomiliki mashamba ya mirungi na ambao wamekimbia nyumba zao wajisamishe.

“Tutapambana nao kuhakikisha wale wote waliokimbia nyumba zao na kuwatesa wana familia, hasa watoto wanakamatwa. Eneo lote wameacha nyumba watoto wanalala nje,” alisema.

“Kitendo cha kukimbia kinatuonyesha wazi wanahusika na kilimo cha mirungi. Tutaendelea kulifanyia doria eneo hilo kuhakikisha waliokimbia wamepatikana,” alisema kamanda huyo.

Kamishina wa Operesheni wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Mihayo Msikhela alisema operesheni hiyo ni endelevu na itahamia mikoa ya Arusha, Tanga, Songwe na Kagera.

Kamishina huyo alisema wilaya ya Same ndiyo inayoongoza kwa kilimo cha mirungi kwa ajili ya kuiuza.

“Hiyo mikoa yote tutaifikia. Wameutoa huo mmea msituni na kuja kuuotesha kwenye mashamba yao. Tutawafikia tu na adhabu itatolewa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Kamishina huyo alisema eneo hilo la milimani lina rutuba na linafaa kwa kilimo cha kahawa, viazi mbatata, mahindi, migomba na miwa.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata