UNAIJUA SIRI YA MAALIM SEIF NA KARUME?

Mtandao huu hivi karibuni ulifanya mahojiano na Katibu Mkuu wa CUF ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim Seif Sharif Hamadi nyumbani kwake Ilala jijini Dar es Salaam. Ungana nasi katika mahojiano hayo ufahamu mengi aliyoyasema:
Swali: Suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) lipo kwenye katiba ya Zanzibar au yalikuwa ni makubaliano ya mdomo?
Jibu: Serikali ya Umoja wa Katiba (SUK) imo ndani ya katiba, isipokuwa hii ya sasa hivi ya Dk. Ali Mohammed Shein haipo, tena basi sisi hatuitambui kwa sababu imepora ushindi wetu.
Katiba ya Zanzibar inasema wazi kwamba Muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Marekebisho ya 10 ya Katiba ni kuwa na Rais Mtendaji, Makamu wa Kwanza wa Rais atakayeteuliwa na rais baada ya kushauriana na chama cha siasa kilicho pata nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa rais, makamu wa pili wa rais atakayeteuliwa na rais kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka katika chama cha siasa anachotoka rais.
Pia, rais kwa kushauriana na makamu wote wawili atateua mawaziri kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kuzingatia uwiano wa viti vya majimbo kwa vyama vya siasa vilivyomo ndani ya Baraza la Wawakilishi lakini serikali hii ya Shein imekiuka hayo yote kwani hakuna chama kilichokidhi matakwa hayo ya katiba. Swali: Baada ya nyinyi yaani wewe na  Rais Amani Abeid Karume kukubaliana ni nini kilifuata? Jibu: Pamoja na kuunda jopo la watu sita, bado tukaona suala hili lipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi ili lipitishwe kisheria.
Kule lilipelekwa kama hoja na Mheshimiwa Abubakar Khamisi Bakary likajadiliwa na likapitishwa. Lakini hata hivyo, ikaonekana lazima lipelekwe kwa wananchi likapigiwe kura.
Bunge likaunda kamati ya watu sita kusimamia jambo hilo na watu hao ni Ali Mzee Ali (CCM), Abubakar Khamisi Bakary (CUF), Ali Abdallah Ali (CCM), Haji Omar Kheri (CUF), Nassor Ahmed Mzrui (CUF) na Zakiya Omar Juma (CCM), walifanya kazi nzuri sana wananchi wa Zanzibar walipiga kura ya maoni siku ya Jumamosi Julai 31, 2010.
Kura hiyo ilikuwa na lengo la kutafuta ridhaa ya wananchi katika kuamua iwapo wanalikubali wazo la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010.( Matokeo hayo yalitoa ushindi wa kura za NDIO kwa asilimia 66.40% dhidi ya kura za HAPANA asilimia 33.90%)
Swali: Kuna madai kuwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume ni rafi ki yako na mfuasi wa CUF, je kuna ukweli wowote katika hili?
Jibu: Siyo kweli kwamba Rais Mstaafu Amani Karume ni mfuasi wa Cuf isipokuwa siri iliyopo ni kweli kwamba Karume anapenda amani na maendeleo ya watu wa Zanzibar kwa sababu ndiye tuliyejadiliana naye na kukubaliana kuundwa kwa serikali ya kitaifa tukaacha itikadi zetu. Hii siri wengi hawajui.
Swali: Kama Karume siyo CUF ilikuwaje hadi mkakubaliana kuunda serikali ya kitaifa?
Jibu: Siku moja tukiwa msibani tulionana na mzee Hassani Nassoro Moyo, tukajadili kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar, akasema kwa nini tusikae meza moja kuondoa kasoro zetu za kisiasa ili nchi isonge mbele? Nilimwambia nitakwenda kwake kuonana naye. Kweli nilikwenda na tukazungumza. Akasema atakwenda
kuonana na Rais Amani Karume ampe ujumbe huo, alikwenda na baada ya siku chache akaniambia rais amekubaliana na wazo hilo hivyo atapanga siku mkutane. Kweli siku moja nikapigiwa simu kualikwa na rais ikulu, nikaenda na kujadiliana kuhusu serikali ya kitaifa. Tulikubaliana tuunde kamati ya watu sita, watatu wa CCM na watatu wa CUF ili wapate njia ya kufanya.
Swali: Kwa mtazamo wa CCM, Maalim hawataki uwe rais wa Zanzibar wakidai eti unataka kuwarudisha Waarabu. Unaweza kutoa ufafanuzi wa hofu hii ya chama tawala?
Jibu: Kwanza ni kweli kwamba CCM hawataki mimi niwe rais wa Zanzibar kwa sababu nawajua, wana hofu kwamba nikiwa rais nitalipa kisasi kutokana na mambo mabaya waliyonifanyia lakini nasema kwa dhati kutoka moyoni kwangu kwamba hilo siwezi kulifanya.
Mimi nawaambia ninachoangalia ni maendeleo ya watu wa Zanzibar, basi, hofu ya kisasi waondoe. Lakini hata hicho kinachosemwa kwamba nitawarudisha Waarabu, ni Mwarabu gani atakayerejea Zanzibar? Hizo ni propaganda tu za CCM. Historia ya visiwa vyote duniani vina watu mchanganyiko, hata ukienda Mauritius, Seycheles, Comoro ni hivyo.
Swali: Wewe unamfahamu zaidi Profesa Lipumba kuliko wengi wanavyofi kiri, unaweza kutueleza ni nini hasa kimembadili Lipumba kuwa alivyo?
Jibu: Profesa Ibrahimu Lipumba nimeanza kumfahamu tukiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka mingi sana iliyopita, hivyo ni kweli namfahamu sana.
Tukiwa chuo tulikuwa kwenye umoja wa dini ya Kiislamu pale chuoni. Kwenye harakati za kisiasa ni mimi ndiye niliyependekeza aitwe atusaidie kwanza kama mshauri wa chama, baadaye akawa mwenyekiti. Sasa ukiniuliza kwa nini amebadilika, siwezi kukupa jibu, hilo anatakiwa alijibu yeye mwenyewe.
Swali: Huoni kwamba mgogoro wenu umesababisha chama kugawanyika?
Jibu: Chama hakikugawanyika, mgogoro uliopo umetengenezwa na msajili wa vyama kwa sababu Lipumba amekataliwa na vikao halali vya chama na siyo na Maalim Seif, kwenye mkutano mkuu wa CUF una wajumbe kama 475 waliomkataa na kusema afukuzwe uanachama ni wengi na waliosema asifukuzwe ni 14 tu.
Swali: Kwa mara ya kwanza Cuf ilipata wabunge wengi Bara katika uchaguzi, unadhani hii ni sababu ya kukubalika kwa chama hicho upande wa Bara au kilisaidiwa zaidi na muungano wa Ukawa?
Jibu: Vyote viwili, chama kimekubalika lakini Ukawa umesaidia vyama vyote vilivyoungana. Huko nyuma tulikuwa tukiwashinda CCM lakini sisi kura zetu zilikuwa zikigawanywa, sasa Ukawa umesaidia CUF na Chadema na hata NCCR ndiyo maana tumepata wabunge, uchaguzi ujao tutapata wabunge wengi zaidi.
Itaendelea...

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata